• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 8:55 PM
Mkurugenzi wa zamani wa makavazi Mzalendo Kibunjia ashtakiwa kwa wizi wa Sh491m

Mkurugenzi wa zamani wa makavazi Mzalendo Kibunjia ashtakiwa kwa wizi wa Sh491m

Na RICHARD MUNGUTI

MKURUGENZI mkuu wa zamani wa makavazi ya kitaifa (NMK) Mzalendo Kibunjia ameshtakiwa kwa ulaghai wa Sh491 milioni.

Kibunjia alishtakiwa pamoja na Stanvas Ongalo Opija (mkurugenzi wa masuala ya usimamizi), Oliver Okinyi Rabour (afisa wa masuala ya teknolojia na malipo) Wycliffe Odhiambo Ongata (mmiliki wa kampuni ya Galmalink Enterprises) na Oscar Mwaura (mmiliki wa kampuni ya Altcoms Limited).

Kibunjia na wenzake wanne walishtakiwa Jumanne kwa kuwalipa wafanyakazi hewa zaidi ya Sh491.2 milioni kutoka kwa akaunti za NMK.

Washtakiwa hao walikabiliwa na mashtaka 10 walipofikishwa mbele ya hakimu mkuu Victor Wakhumile, katika Mahakama ya kuamua kesi za ufisadi Milimani Nairobi.

Katika mashtaka hayo 10 washtakiwa walidaiwa walikula njama za kuifilisi NMK Sh491.2 milioni kwa kuwalipa wafanyakazi hewa.

Bw Wakhumile alifahamishwa washtakiwa walijilipa pesa hizo Sh491.2 milioni kwa miaka kadhaa wakijifanya zilikuwa malipo ya mishahara na marupuru ya wafanyakazi wa NMK.

Walikabiliwa vile vile na kesi ya ufisadi, kutumia vibaya mamlaka ya afisi zao na kupokea pesa za umma kwa njia ya undanganyifu.

Katika mashtaka ya ubadhirifu wa pesa za umma, hakimu alifahamishwa washtakiwa hao walipokea Sh491.2 milioni kutoka kwa akaunti za NMK wakijua wanashiriki uhalifu.

Pesa hizo zililipwa kati ya 2016 na 2022.

Ongata ambaye ni mmiliki wa kampuni ya Galmalink alipokea Sh14,560,446 kutoka kwa Oscar Mwaura na Victor Owuor akijua ni mali ya rushwa.

Washtakiwa waliachiliwa kwa dhamana ya Sh10 milioni na mdhamini mmoja wa kiasi sawa na hicho au walipe dhamana ya pesa tasilimu Sh5,000,000.

  • Tags

You can share this post!

Mtajuta kuturushia makombora, Mkuu wa Jeshi Israel aambia...

Kilio cha mwanamke mgonjwa aliyekwama Saudi Arabia

T L