Mkuu wa Majeshi kuzikwa jinsi alivyoagiza
MKUU wa Majeshi (KDF), Jenerali Francis Omondi Ogolla ambaye aliaga dunia Alhamisi Aprili 18, 2024 katika ajali ya helikopta eneo la Sindar kwenye mpaka wa Kaunti ya Pokot Magharibi na Elgeyo Marakwet atazikwa Jumapili.
Hii ni kulingana na tangazo lililotolewa na familia yake Ijumaa.
Jenerali Ogolla atazikwa nyumbani kwake Mor, Alego, Kaunti ya Siaya.
“Kutokana na jinsi alivyokuwa akiishi maisha ya unyenyekevu, Jenerali Ogolla aliagiza kuwa akifariki, azikwe ndani ya saa 72,”
“Hivyo, familia yeke imechagua Jumapili, Aprili 21, 2024 kuwa siku yake ya kupumzishwa. Jenerali atazikwa nyumbani kwake Mor, Alego, Kaunti ya Siaya,” taarifa kwa vyombo vya habari kutoka kwa familia ya jenerali huyo ilisoma.
Ibada ya ukumbusho pia itaandaliwa katika uwanja wa Ulinzi Sports Complex Langata mnamo Ijumaa, Aprili 26, familia hiyo ilisema.
Ijumaa, wingu la simanzi lilitanda katika eneo la Utange Kaunti ya Mombasa, pale mwili wa marehemu Brigedia Said Swaleh ulipowasili nyumbani kwao majira ya saa nane mchana.
Wanakijiji walikuwa wamesubiri mwili wa mwendazake, ambaye alipoteza maisha yake katika ajali ya ndege ya jeshi, iliyopata ajali katika eneo la Kaben, Pokot magharibi pamoja na maafisa wengine tisa akiwemo mkuu wa majeshi ya ulinzi jenerali Francis Ogolla.
Baada ya sala, mwili wake ulisafirishwa hadi nyumbani kwake eneo la Bomani huko Kikambala, kaunti ya Kilifi ambapo ulizikwa.