Habari za Kitaifa

Mmiliki wa kampuni ya gesi iliyolipuka kukaa ndani siku 21

February 7th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA RICHARD MUNGUTI

MMILIKI wa kiwanda cha gesi cha Embakasi ambako mlipuko ulitokea na kusababisha watu sita kufariki na zaidi ya 300 kujeruhiwa, atasalia korokoroni kwa siku 21.

Bw Derick Kimathi na maafisa watatu wa Mamlaka ya Uhifadhi wa Mazingira (Nema) watazuiliwa katika kituo cha Polisi cha Embakasi hadi polisi wakamilishe uchunguzi.

Akiagiza washukiwa hao Bw Kimathi mmiliki wa kampuni ya Maxxis Energy Nairobi Limited pamoja na maafisa wa Nema Bw Joseph Makau na Bi Marian Mutete Kioko na Bw David Warunya On’gare wasalie rumande, hakimu mwandamizi Bi Dolphina Alego alisema “kesi hii iko na umuhimu mkubwa kwa umma.”

Bi Alego aliamuru Bw Kimathi, Bw Makau na Bi Kioko wazuiliwe katika kituo cha Polisi cha Embakasi naye Bw Ong’are azuiliwe katika kituo cha polisi cha Capitol ili awe karibu na hospitali kwa vile anaugua.

Hakimu alisema mshukiwa huyo “anahitaji kuwa karibu na hospitali kutokana na hali yake ya kiafya.”

Mawakili Odero Okello na Karathe Wandugi wanaowatetea washukiwa hao, walieleza mahakama Bw Ong’are anahitaji huduma za matibabu na hafai kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Embakasi.

Hakimu alikuwa ameombwa aagize mshukiwa huyo apelekwe katika Hospitali ya Karen kupokea matibabu huku polisi wakiendelea na uchunguzi wao.

Akikubalia ombi la viongozi wa mashtaka Herbat Isonye, Dorcus Rugut, Sonia Njoki na James Gachoka kwamba washukiwa hao wazuiliwe kwa siku 21, hakimu alisema polisi wanahitaji muda kuchunguza kesi hiyo kwa kina.

“Kisa cha kulipuka kwa gesi usiku wa Februari 1 kuamkia Februari 2, 2024, kiliwaacha wengi vinywa wazi na wakiwa wamepigwa na mshtuko na bumbuwazi. Watu sita waliaga dunia na wengine zaidi ya 300 wanauguza majeraha mabaya,” alisema hakimu.

Bi Alego alikubaliana na viongozi wa mashtaka kwamba polisi na maafisa wa asasi mbali mbali za serikali wanahitaji muda kukamilisha uchunguzi wa kina.

Akiwasilisha ombi washukiwa hao wazuiliwe kwa siku 21, Inspekta Mkuu wa Polisi Isack Tenai alimweleza hakimu kwamba “uchunguzi wanaofanya utahusisha asasi kadhaa za serikali.”

Alisema polisi wanawachunguza washukiwa hao kwa mauaji, matumizi mabaya ya mamlaka, kutokuwa na makini na kula njama za kutenda uhalifu.

Pia Insp Tenai alieleza mahakama kwamba bado ufukuzi wa eneo la mkasa unaendelea na polisi wanahofia kuna miili zaidi imefunikwa katika kiwanda hicho.

Hakimu alielezwa kwamba suala hili ni mkasa wa kitaifa na lazima ukweli ujulikane kwa vile maafisa wa hawa wa NEMA lazima waeleze jinsi walipeana leseni kiwanda hicho kistiriwe kati kati ya makazi ya watu.

Mabw Gachoka na Isonye na Bi Rugut walisema“korti inapasa kutilia maanani watu walikufa katika mkasa huo na mamia wanauguza majeraha. Mamia wanahitaji ushauri kutokana na mshtuko na pia upasuaji wa maiti haujafanywa.”

Hakimu alielezwa bado polisi hawajafikia uamuzi mashtaka watakayowafungulia washukiwa.

“Uchunguzi ukikamilishwa polisi watajua mashtaka watakayowashtaki washukiwa hao,” Bi Rugut alimweleza hakimu.

Pia Bw Isonye alieleza mahakama usalama wa washukiwa unapasa kutiliwa maanani kwa “vile wakazi wa Embakasi wangali na hasira nao washukiwa.”

Lakini mawakili Wandugi na wenzake walipinga ombi hilo wakisema “polisi wanapasa kuwa wamekamilisha uchunguzi na kwamba ombi la siku 21 washukiwa wakiwa ndani halina mashiko kisheria.”

Bw Okello,Bw Wandugi na mawakili mwingine Kavita Mwanzia na Dkt Duncan O’Kubasu walieleza mahakama kwamba washukiwa hao wanaweza kuachiliwa kwa dhamana kisha waagizwe wawe wakipiga ripoti kwa polisi mara mbili au tatu kwa wiki.

Akitoa uamuzi hakimu alisema washukiwa hao wanapasa kuzuiliwa kwa siku 21 “kwa mlipuko huo uliopelekea watu kuangamia ni janga la kitaifa na polisi wanahitaji muda kukamilisha zoezi lao la kuchunguza.”

“Ombi la Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Renson Ingonga kupitia kwa Bi Rugut, Bi Njoki na Mabw Gachoka na Isonye liko na mashiko kisheria na washukiwa watazuiliwa siku 21 kusaidia polisi katika uchunguzi,” alisema Bi Alego.

Hakimu aliamuru washukiwa wazuiliwe hadi Februari 28, 2024.