Mnaagizaje mchele na vuno letu halijapata wanunuzi, wakulima Mwea wachemkia serikali
WAKULIMA wa mpunga katika mradi mkubwa wa unyunyuzaji wa Mwea wamepinga vikali agizo la serikali kuruhusu uagizaji wa tani 500,000 za mchele kutoka nje ya nchi bila ushuru kabla ya Desemba mwaka huu.
Agizo hilo lilitolewa kupitia tangazo rasmi la serikali na Waziri wa Fedha na Mipango ya Kiuchumi, Bw John Mbadi, kufuatia mapendekezo kutoka kwa Wizara ya Kilimo.
Hata hivyo, wakulima wamesema hatua hiyo itawavunja moyo zaidi kwani tayari wana zaidi ya magunia 50,000 ya mchele yasiyo na soko katika ghala la chama cha ushirika cha wakulima wa mchele Mwea mjini Ngurubani.
“Kwa nini kuagiza mchele kutoka nje ilhali wetu wa hapa hauuzwi?” alihoji mkulima mmoja, Bw Pius Njogu, akiongeza kuwa mchele wa bei nafuu kutoka nje utaharibu kabisa soko la zao lao.
Seneta wa Kirinyaga Kamau Murango, alikashifu vikali agizo hilo la serikali akilitaja kama lililokosa mwelekeo.
“Serikali iliahidi kununua magunia yote 50,000 ya mchele kutoka kwa wakulima lakini hadi sasa haijatekeleza hilo. Badala yake, inatoa maagizo ya kukandamiza wakulima,” alisema.
Seneta huyo alisema wakulima huchangia sana katika maendeleo ya taifa na serikali inapaswa kuwasaidia kupata masoko badala ya kuwaongezea matatizo.
Licha ya malalamishi hayo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Chakula na Kilimo (AFA) Dkt Bruno Linyiru, alitetea mpango huo akisema mahitaji ya kitaifa ya mchele ni tani 1.3 milioni kwa mwaka, huku uzalishaji wa humu nchini ukiwa tani 264,000 pekee.
“Huu si wakati wa kwanza Kenya kuagiza mchele kutoka nje. Tutaendelea kufanya hivyo hadi tutakapojitosheleza,” alisema Dkt Bruno.
Mwea huzalisha asilimia 80 ya mchele unaotumiwa humu nchini, lakini wakulima wanasema jitihada zao zinafifishwa na maamuzi ya serikali yasiyowazingatia.
TAFSIRI: BENSON MATHEKA