Habari za Kitaifa

Mnazi, busaa, muratina kuuzwa bila leseni mswada ukipita bungeni

Na COLLINS OMULO September 21st, 2024 Kusoma ni dakika: 1

WATENGENEZA pombe za kitamaduni kama vile mnazi, busaa na muratina huenda wakaziuza bila kuhitajika kuchukua leseni, ikiwa mswada mpya ulioko bungeni utapitishwa kuwa sheria.

Pendekezo hilo liko kwenye mswada uliopendekezwa na Seneta Maalum Raphael Chimera.

Mswada huo wa Marekebisho ya Sheria kuhusu Udhibiti wa Pombe wa 2024 unalenga kuondoa hitaji la watengenezaji wa pombe za kitamaduni kulipia ada za kupata leseni.

Kulingana na Seneta Chimera, pombe za kitamaduni zina umuhimu wa kimila katika jamii mbali mbali ambazo huzitengeneza tangu miaka ya nyuma.

Pombe hizo hutumika nyakati za sherehe za kitamaduni kama vile utoaji mahari, upashaji tohara, uhitimu kuingia barabara za wazee, maridhiano miongoni mwa watu wa familia moja, maombi ya kuvutia mvua na hafla za kubariki watoto na mifugo.

Kwa hivyo, anasema Seneta Chimera, sio haki kwa serikali kudhibiti biashara ya pombe za kitamaduni kwani zina umuhimu mkubwa katika jamii husika.

“Pombe za kitamaduni ni nguzo muhimu katika shughuli na hafla mbalimbali katika jamii kadhaa za Kenya. Kwa hivyo, sio haki kwa watengeneza na wauzaji wa pombe hizo kuhitajika kulipia leseni au kutozwa ada nyinginezo,” akasema.

Kupitia mswada huo, Bw Chimera anataka pombe za kitamaduni zitahalalishwe kisheria na kuchukuliwa kama vinjwaji vya kawaida vinavyotengenezwa kwa kutumia malighafi na mbinu za kiasili.