Moi alikataa pendekezo la kuua Raila kwa kukosoa utawala wake, Mkuu wa Habari Ikulu afichua
ALIYEKUWA Rais wa pili wa Kenya, Daniel arap Moi alikataa pendekezo la afisa wa usalama la kumuua Raila Amolo Odinga, aliyekuwa mmoja wa wapinzani wake wakuu, msaidizi wa zamani wa Ikulu amefichua.
Tukio hilo ni mojawapo ya maamuzi muhimu zaidi yaliyofanywa na rais huyo katika uongozi wake, yaliyoonyesha ukomavu wake wa kisiasa na maono ya kuleta umoja nchini.
Lee Njiru, aliyekuwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari Ikulu, anasimulia tukio hilo kwa kina. Kwa maneno yake, afisa mmoja wa usalama alienda kwa Rais Moi na kumweleza kuwa Raila alikuwa akisababisha matatizo makubwa serikalini na aliomba ruhusa ya kumaliza usumbufu huo kwa kumuua.
“Mzee Moi aliwahi kuniambia,” alianza Njiru kwa sauti tulivu lakini yenye uzito wa hisia, “kwamba afisa mmoja mkuu wa usalama alienda kwake na kusema, ‘Mheshimiwa Rais, kwa nini huyu mtu Raila anakusumbua hivi? Nipe ruhusa tumalizane naye.’ Lakini Mzee alimwangalia, akatikisa kichwa na kusema kwa msimamo thabiti: La hasha.”
“Ndio,” anasema polepole, “wapo waliotaka Raila aondolewe kabisa. Lakini Mzee Moi alikataa. Alisema: “Aendelee tu. Kenya inahitaji watu kama yeye.’”
Kulingana na Njiru, uamuzi huo ulionyesha ukomavu wa kisiasa wa Moi na umuhimu wa Raila katika demokrasia ya Kenya.
“Raila,” anasema, “alikuwa sehemu muhimu katika injini ya siasa za Kenya — mtu aliyepinga mamlaka, kuchochea mijadala, na kusukuma nchi hii kubadilika
Bw Njiru anasema kuwa uamuzi huu uliashiria busara na uongozi wenye hekima wa Moi, ambaye aliweza kutambua kuwa siasa bora ni zile zinazoendeshwa kwa majadiliano na kuheshimu maoni tofauti.
Kulikuwa na watu ndani ya serikali waliopendelea mbinu kali dhidi ya wapinzani wa kisiasa kama Raila. Lakini Rais Moi alikataa hilo kwa kauli thabiti na kuonyesha kuwa badala ya kutumia nguvu, serikali ingeendelea kuweka mkazo katika mazungumzo na upatanishi.
Njiru anafafanua kuwa Moi alikuwa na mtazamo mpana zaidi kuliko siasa za kawaida. Alielewa kuwa Raila alikuwa ni chombo cha mabadiliko, mtu mwenye msimamo mkali na ambaye hakuhofia kupinga maamuzi yasiyo sawa.
“Raila alikuwa nguzo muhimu katika siasa za Kenya,” anaeleza Njiru, “alichochea mijadala, akatoa changamoto kwa utawala, na kusaidia Kenya kukua kisiasa.”
Kwa hivyo, kuendelea kwake katika siasa kulihitaji uongozi na watu kuvumilia na kuheshimu maoni tofauti.