Mpaka wa Kenya na Tanzania kero kwa mbegu ghushi kupenyezwa nchini
TAASISI ya Ukaguzi kuhusu Afya ya Mimea Nchini (Kephis) imeelezea wasiwasi wake kuhusu ongezeko la mbegu ghushi zinazovukishwa mpakani na wafanyabiashara wenye ushawishi.
Katika shughuli ya ukaguzi iliyoanza Jumatano, Septemba 4, 2024 kwenye kituo kikuu cha mpakani cha Namanga, maafisa wa Kephis walisisitiza kuwa wamejitolea kuzuia ongezeko la mbegu ghushi nchini.
Kephis inatumia mikakati inayojumuisha vikosi mbalimbali kuokoa sekta ya kilimo kutokana na wafanyabiashara wakora.
Mwenyekiti wa Kephis, Joseph M’uthari, alisema kikosi cha uangalizi kimemakinika katika vituo vyote vya mpakani ili kuzuia mbegu ghushi kuingizwa nchini.
“Timu yetu ya uangalizi imemakinika zaidi kuhakikisha mbegu zote zinazosambazwa nchini zimeidhinishwa na mamlaka husika. Usambazaji wa mbegu ghushi ni pigo kuu kwa sekta ya kilimo nchini,” alisema Bw M’uthari.
Mabwanyenye wanaohusika na mbegu ghushi wanasemekana kupanua shughuli zao katika mataifa jirani hususan eneo la Afrika Mashariki, Kati na Magharibi.
Mkurugenzi wa Kephis, Theophilus Mutui, alisema msako kuhusu mbegu ghushi umeimarishwa sio tu mpakani lakini katika vituo vyote vya kuuzia bidhaa za kilimo.
Hata hivyo, mpaka wa Kenya-Tanzania umezua changamoto kuu katika vita dhidi mbegu feki.
“Tunaimarisha msako kwenye vituo vya mpakani na kote nchini. Tunatoa onyo kali kwa wafanyabiashara wanaoingiza na kusambaza mbegu ghushi nchini,” alisema Bw Mutui.
“Tunaandama baadhi ya washukiwa na tutawakamata hivi karibuni.”
Kephis vilevile inapigia debe mtindo wa wakulima kubadilishana mbegu ili kuimarisha usambazaji wa mbegu bora zenye mavuno tele na kuwakinga kutokana na wafanyabiashara matapeli.
Mtu anayepatikana na hatia ya kusambaza mbegu ghushi atapigwa faini ya Sh 1M, kifungo cha miaka miwili au vyote viwili.
Wafanyabiashara wasiopungua 100 wameshtakiwa katika muda wa mwaka mmoja uliopita, kulingana na takwimu za Kephis.