Mshukiwa mkuu wa mauaji KNH akamatwa na Polisi
Maafisa wa uchunguzi wa mauaji kutoka Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) wamemkamata mshukiwa mkuu wa mauaji ya mgonjwa katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH), jijini Nairobi.
Kulingana na DCI, Kennedy Kalombotole, ambaye amekuwa akilazwa hospitalini humo tangu Desemba 1, 2024, alikamatwa Alhamisi jioni kuhusiana na mauaji ya Edward Maingi Ndegwa, mgonjwa aliyekuwa katika Wodi ya 7B, tangu Julai 11, 2025.
Kwa mujibu wa taarifa ya DCI, muuguzi wa wodi hiyo alimkagua mgonjwa huyo mnamo Alhamisi, Julai 17, saa tano na nusu asubuhi na kupima shinikizo lake la damu. Saa moja baadaye, jamaa wa mgonjwa huyo alimtembelea na kumpata akiwa salama, kabla ya kuondoka saa saba na nusu mchana.
Hata hivyo, kufikia saa nane alasiri, mfanyakazi aliyekuwa akisafisha wodi aligundua damu ikitiririka kutoka shingo ya mgonjwa huyo.
Polisi walifahamishwa mara moja na walipozuru eneo la tukio, walibaini alama za viatu zenye damu kutoka kando ya kitanda cha marehemu hadi katika choo kilicho karibu, kisha hadi chumba cha kando ambacho Kalombotole alikuwa amelazwa.
Ndani ya chumba hicho, maafisa wa DCI walipata jozi ya sapatu za buluu pamoja na shuka lililotapakaa damu. Pia, walipata kisu kilichofungwa kwa glavu.
Vitu hivyo vilikabidhiwa Maabara ya Kitaifa ya Kisayansi kwa uchunguzi wa kina ili kusaidia katika kufanikisha kesi hiyo.
Aidha, uchunguzi wa awali ulifichua kuwa Kalombotole pia ni mshukiwa mkuu katika mauaji ya Gilbert Kinyua Muthoni, mwenye umri wa miaka 40, aliyepatikana ameuawa katika wodi 7C usiku wa kuamkia Februari 7, 2025.
Kufuatia kifo hicho, polisi waliandaa faili ya kesi na kuiwasilisha kwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP). Hata hivyo, ODPP aliagiza uchunguzi zaidi ufanywe ili kuimarisha ushahidi wa kesi hiyo.
Kwa sasa, Kalombotole anazuiliwa na polisi akisubiri kufikishwa mahakamani baada ya kukamilika kwa uchunguzi.