Habari za Kitaifa

Msije na rasta kichwani, waambiwa wanafunzi wa St George’s katika masharti makali

Na KEVIN CHERUIYOT September 16th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

BAADA ya kufungwa kwa wiki moja, Shule ya Upili ya Wasichana ya St George’s, Nairobi imetangaza kukamilisha mipango ya kuwaruhusu wanafunzi kurejelea masomo kuanzia leo, Jumanne.

Shule hiyo ilifungwa Jumatatu wiki iliyopita baada ya wanafunzi kuzua rabsha nyakati za usiku.

Wanafunzi watarejea kwa awamu, huku wanafunzi wa Kidato cha Nne wakipewa kipaumbele.

Katika barua iliyotumwa kwa wazazi na nakala yake kutumwa kwa wakuu wa elimu, Mwalimu Mkuu Assumpta Mwangi alisema uamuzi wa kufunguliwa kwa shule ulifikiwa kwa pamoja na Bodi ya Wasimamizi na Wizara ya Elimu.

“Zingatia kuwa wanafunzi wa Kidato cha Nne wanatarajiwa kuripoti shuleni kama ifuatavyo; Jumanne Septemba 16 kufikia saa nne asubuhi (10 am), Kidato cha Nne P, G, W na Y.

Jumatano, Septemba 17 kufikia saa nne asubuhi, Wanafunzi wa Kidato cha Nne R, K, N na S,” ikaeleza barua hiyo.

Wazazi na walezi wameshauriwa kwamba ni sharti waandamane na watoto wao ilivyoratibiwa kwenye kanuni za shule.

Vile vile, shule imewataka wazazi na wanafunzi kuhakikisha wamefumua nywele zao zilizosukwa na wachane nywele zao vizuri kabla ya kuingia shuleni.

Aidha, wazazi wametakiwa kukamilisha masalio ya karo na kwamba wanafunzi ambao hawajakamilisha kulipa karo hawataruhusiwa kurejelea masomo.

Bi Mwangi hakubainisha ni lini wanafunzi wa madarasa mengine watarejelea masomo japo duru ziliambia Taifa Leo kwamba watarejea juma lijalo.

Wiki jana, Mkurugenzi wa Elimu katika Kaunti ya Nairobi, aliongoza mazungumzo na wanachama wa Bodi ya Wasimamizi wa Shule hiyo ya St George’s.

Idara ya Ubora imetakiwa kuendesha uchunguzi kubaini chanzo cha fujo za wanafunzi zilizopelekea kufungwa kwa shule.

Lakini uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa hali hiyo ilisababishwa na changamoto kadhaa zinazokumba shule hiyo ikiwemo njia ambazo shule hutumia kuadhibu wanafunzi.

Aidha, usimamizi wa shule umelaumiwa kwa kufeli kusikiza malalamishi ya wanafunzi.