Msithubutu kubadilisha chochote kuhusu ushuru mpya, wizara yaambia Bunge
EDWIN MUTAI NA BENSON MATHEKA
HAZINA ya Kitaifa inataka Bunge kupitisha mapendekezo ya ushuru unaoumiza raia yaliyo katika Mswada wa Fedha, 2024 ili serikali iweze kupata mapato ya kulipa deni la Kenya ambalo kwa sasa linafikia Sh11.2 trilioni.
Hazina ya Taifa ilitetea ushuru huo mkubwa ikisema kuwa hali ya deni la Kenya inatarajiwa kuwa mbaya zaidi katika muda wa kati.
Katibu wa Hazina Dkt Chris Kiptoo aliambia Kamati ya Bunge ya Kitaifa ya Fedha na Mipango ya Kitaifa kwamba deni lilifikia asilimia 72 ya Pato la Taifa (GDP) ambayo ni juu zaidi ya asilimia 55 iliyowekwa katika sheria ya fedha za umma.
Dkt Kiptoo aliambia kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Molo Kuria Kimani kwamba kiwango cha madeni kilifanya Wakenya zaidi kuwekwa katika makundi ya kulipa ushuru.
Mswada huo unapendekeza kutozwa ushuru bidhaa muhimu ikiwa ni pamoja na kutoza mkate ushuru wa ziada wa thamani (VAT) wa asilimia 16 na asilimia 25 kwa mafuta ghafi na yaliyosafishwa ya kupika.
Mswada huo pia unapendekeza kutoza VAT ya asilimia 16 huduma za kifedha na huduma za kutoa na kutuma pesa kutoka asilimia 15 ya sasa hadi asilimia 20.
Pia unapendekeza ushuru wa kila mwaka wa asilimia 2.5 wa magari kulingana na thamani ya gari na ushuru wa mazingira wa Sh150 kwa plastiki.
Hazina ya Taifa inataka kupata angalau Sh58 bilioni kutoka ushuru wa magari. Mswada wa Sheria ya Fedha, 2024 unalenga kukusanya jumla ya Sh302 bilioni ili kufadhili bajeti sehemu ya Sh3.9 trilioni ya 2024/25.
Dkt Kiptoo aliwaambia wabunge kwamba Kenya itahitaji Sh1.1 trilioni kulipa riba ya deni katika mwaka wa kifedha unaoanza Julai 1, 2024.
“Tunazungumzia Sh1.1 trilioni ambazo tunahitaji kulipa kama riba ya mikopo yetu. Ni lazima tulipe deni letu, vinginevyo tutatozwa faini kwa kushindwa kulipa. Ina maana kwamba kwa kila Sh10 ambazo Mamlaka ya Ushuru ya Kenya (KRA) inakusanya, Sh6 zinaenda kulipa deni hilo,” Dkt Kiptoo alisema.
“Lazima tubadilishe hali hii kufikia 2028. Hatua za ushuru katika Mswada wa sasa wa Fedha wa 2024 zinalenga hili. Tumepunguza matumizi kwa takriban Sh300 bilioni.”
Dkt Kiptoo alisema deni la nchi liliongezeka kutoka hatari ndogo mwaka wa 2014 hadi hatari ya wastani mwaka wa 2018 na lilishuka hadhi mwaka wa 2020 hadi kundi la hatari zaidi.
Kamati hiyo, hata hivyo, ilimtaka Dkt Kiptoo kueleza ni kwa nini hatua za ushuru mwaka huu zimeshindwa kutimiza malengo ya kukusanya mapato.
Hii ni baada ya Dkt Kiptoo kuwaambia wabunge kuwa Sheria ya Fedha, 2023 ilitarajiwa kukusanya Sh214 bilioni lakini KRA imekusanya Sh131 bilion pekee.
“Kuhusu Ushuru wa Nyumba, tumekusanya Sh47.5 bilioni sawa na asilimia 80 ya lengo la jumla la Sh59.5 bilioni. Huenda tukafikia asilimia 90 kufikia mwisho wa Juni,” Dkt Kiptoo alisema