Habari za Kitaifa

Msukosuko mpya watikisa ndoa ya ODM na UDA

Na JUSTUS OCHIENG’ November 26th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

SERIKALI jumuishi iliyoanzishwa na Rais William Ruto kwa ushirikiano na marehemu Raila Odinga sasa inakumbwa na msukosuko mpya, ikitikiswa na tofauti za wazi, tamaa zinazogongana za kisiasa, jumbe zinazokinzana na vitisho vikali kutoka kwa viongozi wa ngazi za juu kutoka pande zote mbili.

Kile kilichoanza kama jitihada thabiti za kuleta utulivu nchini kufuatia maandamano makubwa ya Gen Z mnamo Juni mwaka jana, sasa kinajaribiwa na misimamo mikali, matarajio yanayokwenda kinyume na pengo linaloongezeka kati ya ahadi za hadharani na mikakati ya chini kwa chini.

Kuanzia vurugu za kampeni za uchaguzi mdogo wa Kasipul hadi madai ya kupatiwa nyadhifa za juu 2027, hadi baadhi ya viongozi wa ODM kufufua lugha ya maandamano ya umma, pamoja na Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna kudai kutishiwa kuondolewa uongozini na kundi linalomuunga mkono Rais Ruto —serikali hiyo jumuishi sasa inapambana kudumu.

Bw Sifuna alidai kuwa kambi ya Rais Ruto ilipanga “kumnyamazisha” wakati wa sherehe za ODM@20 zilizofanyika Mombasa.

Aliongeza kuwa yuko tayari kushirikiana na kiongozi yeyote “atakayesaidia kumwondoa Rais Ruto madarakani,” kauli iliyoibua tashwishi zaidi kuhusu uthabiti wa serikali jumuishi.

“Nilikuwa KICC wakati ODM ilisaini makubaliano na chama cha UDA, ajenda ya vipengee 10, lakini bado utekaji nyara na mauaji ya vijana yanaendelea nchini bila kujali makubaliano hayo,” aliongeza.

Kila upande sasa unazungumza kwa sauti kubwa wakati mwingine hata dhidi ya washirika wao hali inayozua swali kuhusu mwelekeo wa serikali na nchi kwa ujumla.

Seneta wa Nandi Samson Cherargei (UDA) pia ametoa onyo kwa ODM, akisema kwamba ingawa UDA imejitolea kuendeleza ushirikiano huo, kuna mipaka ambayo ODM lazima ikubali, hasa kuhusu urithi wa uongozi 2027 na kugawana madaraka.

“Tuko ndani ya serikali jumuishi, lakini kuna viti viwili ambavyo havijadiliwi — cha Rais William Ruto na cha Profesa Kithure Kindiki,” alisema.

Bw Cherargei alisisitiza kuwa kuelekea mchakato wa miungano mipya ya 2027–2032, UDA inamtambua mgombea mwenza mmoja pekee.

“Naibu wa Rais wa Mheshimiwa William Ruto ni Profesa, Seneta Kithure Abraham Kindiki,” alisema.

“Kwa hiyo nawaambia wenzetu katika serikali jumuishi, viti viwili vya juu vimejazwa mnaweza kuomba vingine.”

Kauli hizo zilitafsiriwa kama pigo la mapema dhidi ya msukumo mpya wa ODM kutaka wadhifa wa Naibu Rais 2027 alivyotamka hadharani kiongozi wa ODM, Dkt Oburu Oginga.

Dkt Oginga alisema ODM haitakubali nafasi iliyo chini ya Naibu Rais katika mazungumzo ya 2027.

“Tusipopata wadhifa wa juu, basi isiwe chini ya wadhifa wa pili kwa ukubwa. Huo ndio msimamo wangu,” alisema.

Lakini ni uchaguzi mdogo wa Kasipul ambao umeanika wazi zaidi migongano ndani ya serikali jumuishi. Kwa upande wa mashinani, viongozi wa ODM wanasema washirika wao wanaonekana kuvuruga umoja ambao muungano huo unadaiwa kuwakilisha kitaifa.

Mbunge wa Homa Bay Mjini Peter Kaluma alilalamikia kile alichokitaja kuwa “jumbe zinazochanganya” kutoka kwa wanasiasa wa UDA wanaomuunga mkono mgombea huru badala ya mgombea rasmi wa ODM, Bw Boyd Were.

“Kasipul, baadhi ya wenzetu katika serikali jumuishi wanampigia debe mgombea huru na wanachanganya wapiga kura wetu,” alisema.

Alimshtumu aliyekuwa Gavana wa Migori Okoth Obado, ambaye sasa ni mratibu wa UDA Nyanza, kwa “kusafiri kutoka Migori kumpigia debe Philip Aroko,” ambaye ni mgombea huru.

Aliorodhesha matukio kadhaa aliyoyaita “ya kusikitisha.” “Odoyo Owidi (mwanaharakati wa UDA) anampigia debe mgombeaji huru na kututusi. Aliyekuwa Gavana wa Nairobi Evans Kidero pia amekutana na Aroko — wanatoa picha gani kwa watu wetu?” alihoji.

Mgawanyiko huu unaonyesha wazi kuwa serikali jumuishi ya Ruto–Raila inazidi kulemewa na maslahi yanayokinzana, ikizua swali kuu: Je, ushirikiano huu utadumu hadi 2027, au ni suala la muda tu kabla ya kuporomoka?

Alimtaja mgombeaji huru huyo kuwa “mshukiwa mkuu wa mauaji ya Ong’ondo Were,” akisema hali hiyo inawatisha wakazi na kuidhoofisha ODM.