• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 2:32 PM
Mswada wa nyumba: Azimio watishia kurejelea maandamano, kuelekea mahakamani

Mswada wa nyumba: Azimio watishia kurejelea maandamano, kuelekea mahakamani

NA CHARLES WASONGA

WABUNGE wa Azimio La Umoja-One Kenya Jumatano alasiri waliondoka bungeni kwa hasira baada ya marekebisho waliowasilisha kwa Mswada wa Nyumba za Gharama Nafuu wa 2023 (AHB, 2023) kuangushwa na wenzao wa Kenya Kwanza.

Wakiongozwa na Kiranja wa Wachache Junet Mohamed, wabunge hao walidai Kenya Kwanza inatumia udikteta kulazimisha kupitishwa kwa mswada huo bila kufanyiwa marekebisho ya kuzuia kunyanyaswa zaidi kwa Wakenya.

“Wabunge wa Azimio waliwasilisha marekebisho kadhaa Jumanne na Jumatano asubuhi. Lakini sasa inaonekana kuwa kuna amri kutoka kwa wakuu wa Kenya Kwanza kule Naivasha kwamba mswada huu upitishwe bila kufanyiwa marekebisho yoyote,” Bw Mohamed akawaambia wanahabari nje ya ukumbi wa mjadala akiandamana na wabunge 20 wa Azimio.

“Kwa hivyo, tumeondoka ukumbini kwa sababu hatutaki kushiriki katika mchakato wa kupitishwa kwa mswada unaokiuka Katiba na kuwaumiza Wakenya wanaozongwa na gharama ya juu ya maisha,” akaongeza mbunge huyo wa Suna Mashariki.

Kulingana na Bw Mohamed, serikali kuu imeteka Bunge ili lipitishe mswada huo haraka.

“Huu Mswada haufaidi wafuasi wa Kenya Kwanza pekee bali Wakenya wote,” akaeleza.

Aliongeza kuwa wabunge wa Azimio waliounga mkono mswada huo katika awamu ya pili walitishwa na serikali ya Kenya Kwanza.

“Nilikutana na wabunge wetu waliopigia kura mswada huo. Nilitaka kuwaadhibu lakini wakalia na kufichua na kuelezea jinsi walivyotishwa kuunga mkono mswada huo kandamizi,” akaongeza.

Mbunge Maalum John Mbadi alimshutumu Rais William Ruto kwa kutumia udikteta kuharikisha kupitishwa kwa mswada huo.

“Kwa hivyo, sisi kama Azimio tumeamua kuwa tutawasilishe kesi mahakamani kuzuia utekelezaji wa mswada huo unaopania kuhalalisha utozaji wa ushuru haramu wa nyumba kutoka kwa wafanyakazi. Aidha, tutarejelea maandamano kupinga mswada huu,” akatisha Bw Mbadi.

Mbunge wa Rarieda pia alilaani serikali kwa kuharakisha kupitishwa kwa mswada huo “kwa namna inayoibua utata wa kisheria.”

“Ni moyo huu wa mbio uliosababisha marekebisho ya Azimio kwa mswada huo kuangushwa,” akaeleza.

Baadhi ya marekebisho yaliyoangushwa na wabunge wa Kenya Kwanza ni yale yaliyowasilishwa na wabunge Millie Odhiambo (Suba Kaskazini), Clive Gesairo (Kitutu Masaba, ODM), na Antony Oluoch (Mathare) kwamba sehemu ya 4 ya Mswada huo unaopendekeza utozaji wa ushuru wa nyumba ifutiliwe mbali.

Badala yake, wabunge hao walitaka mpango huo wa Ujenzi wa Nyumba za Gharama Nafuu ufadhiliwe kupitia pesa za walipa ushuru wala sio ushuru wa kima cha asilimia 1.5 kwa mishahara ya wafanyakazi kila mwezi.

Aidha, pendekezo la Mbunge wa Seme Dkt James Nyikal kwamba ushuru huo utozwe mishahara halisi (net salary) ya wafanyakazi bali sio mshahara wa jumla uliangushwa na wabunge wa Kenya Kwanza (KKA) wakiongozwa na Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wah.

Aidha, marekebisho kadhaa yaliyowasilishwa na Mbunge wa Githunguri Gathoni Wamuchomba (UDA), ambaye ameasi mrengo wa KKA, pia yaliangushwa.

Baadhi ya mapendekezo ya Bi Wamuchomba ni kwamba Shirika la Kitaifa la Nyumba (NHC) ndilo lisimamie fedha za mpango huo wa ujenzi wa nyumba bali sio bodi mpya itakayobuniwa kutokana na mswada huo wa AHB, 2023.

Lakini hata baada ya wabunge wa Azimio kuondoka ukumbini, mbunge wa Funyula Christopher Oundo na Bi Wamuchomba walisalia bungeni kuendelea kupambana na wenzao wa mrengo wa KKA.

Hata hivyo, Mswada huo ulipitishwa pamoja na marekebisho yaliyopendekezwa na kupitishwa na wabunge hao.

Na sasa mswada huo utapitishwa hadi bunge la Seneti ambako utashughulikiwa na kupitishwa kabla ya kuwasilishwa kwa saini ya Rais Ruto.

  • Tags

You can share this post!

Bondia anayeinukia Lamu afichua ‘bullying’ ilimzindua...

Wachuuzi wanne washtakiwa kuuza dawa ‘feki’ ya...

T L