Mtaalamu apuuza madai Kenya imejianika kwa magaidi
CHARLES WASONGA
MBUNGE wa Saboti Caleb Amisi amedai kuwa hatua ya Amerika kuipandisha Kenya kuwa Mshirika wake Mkuu asiye mwanachama wa Kundi la Kujihami la Nato inaiweka Kenya katika hatari ya kushambuliwa na magaidi.
Kwenye ujumbe mfupi kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa X mnamo Jumanne, mbunge huyo aliyechaguliwa kwa tiketi ya ODM anadai kuwa kufuatia hatua hiyo, sasa Kenya itarithi maadui wote wa Amerika.
Kulingana na Bw Amisi katika serikali itatumika kama uwanja wa mvutano wa kisiasa kati ya nchi zenye uwezo mkubwa duniani “hali ambayo itafanya Kenya kulengwa kila mara na magaidi.”
“Kwa kuitambua Kenya kama Mshirika wake asiye mwanachama wa Nato, Amerika imeigeuza Kenya kama kitovu cha vita vya dunia. Tumegeuzwa kuwa uwanja wa mivutano ya kimamlaka miongoni mwa mataifa yenye nguvu na huenda kila mara tukashambuliwa na makundi ya kigaidi, ambayo ni maadui wa Amerika,” Bw Amisi akaeleza.
Mbunge huyo anayehudumu muhula wa pili Bungeni, pia ni mwanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu Ulinzi na Masuala ya Kigeni inayoongozwa na Mbunge wa Belgut Nelson Koech.
“Amerika itatoa tu misaada ya chakula, dawa na silaha baada ya kutokea kwa maovu yanatokanayo na vita. Amerika itapigana na maadui wake kwa kutumia damu ya Kenya sio damu ya Amerika. Tutasambaratishwa kama Ukraine,” Bw Amisi akasema.
Mbunge huyo alisema kuwa Kenya imejipata katika hali hiyo “kutokana na kosa la Uhuru (Uhuru Kenyatta, rais mstaafu) wa kupokeza mamlaka kwa watu wasiofaa na kuchanganyikiwa kwa mrengo wa upinzani wa Azimio.
“Kenya inahitaji ukombozi mpya,” Bw Amisi akasema.
Wakati wa ziara yake rasmi nchini Amerika wiki jana, Rais William Ruto alivuna faidi nyingi baada ya Amerika kuahidi kuipa Kenya mabilioni ya fedha za kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta kadhaa.
Mwenyeji wake, Rais Joe Biden wa Amerika, pia alitoa tangazo la kipekee na kihistoria kwamba Amerika itaitambua Kenya katika Mshirika wake Mkuu asiye mwanachama wa kundi la kujihami la Nato.
Kulingana na Prof Masibo Lumala, ambaye ni mtaalam wa masuala ya kidiplomasia na mahusiano ya kimataifa, hatua hiyo itaiwezesha Kenya kupata msaada wa silaha kutoka Amerika.
“Kwa kupewa hadhi ya Mshirika Mkuu wa Amerika asiye Mwanachama wa Nato, jeshi la Kenya litakuwa likipata misaada ya silaha, mafunzo kwa wanajeshi wetu wa KDF, miongoni mwa misaada mingine ya kiufundi,” akaeleza Prof Lumala, ambaye ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Moi.
Hata hivyo, msomi huyo alifafanua kuwa hadhi hiyo haiipi Amerika wajibu kuingilia kati endapo Kenya itashambuliwa na mataifa mengine.
Kuhusu kauli ya Bw Amisi, Prof Lumala anasema hivi: “Madai hayo hayana mantiki yoyote kwa sababu Kenya imekuwa ikishuhudia mashambulio ya kigaidi hata kabla ya tangazo hilo la Rais Biden.”