Mtachoka tu, hamnitishi na Wan-Tam, Ruto aambia wapinzani
RAIS William Ruto amesisitiza kuwa serikali yake inatekeleza ahadi alizowapa Wakenya na kwamba hataogopa kampeni kwamba atahudumu kwa muhula mmoja tu zinazotolewa na upinzani.
Akizungumza katika Ikulu wakati wa hafla ya kuwezesha kiuchumi makundi ya wakazi wa Nairobi, Rais alisema serikali inaendelea na kazi ya kubadilisha taifa na si kuhusika katika siasa za mgawanyiko.
“Wanajaribu kututisha, kututisha kwa kampeni za muhula mmoja. Ninawaambia kuwa hatutayumbishwa na vitisho hivyo. Tumejizatiti kubadilisha nchi yetu,” alisema Rais Ruto.
Alitoa changamoto kwa upinzani unaoongozwa na Naibu Rais wa zamani Rigathi Gachagua kutoa mpango bora kwa Wakenya kabla ya uchaguzi wa 2027, badala ya kueneza chuki na ubaguzi wa kikabila.
“Tutaunganisha taifa hili kupitia serikali jumuishi inayowajumuisha wote. Serikali inayowaunganisha Wakenya ndiyo itakayopeleka nchi hii mbele, na huo ndio mustakabali wa nchi yetu,” alisema Rais.
Rais pia alisema kuwa uamuzi wa muhula wa viongozi waliochaguliwa utatolewa na wapiga kura wakati wa uchaguzi.
Mkutano huo wa uwezeshaji kiuchumi uliongozwa na viongozi walioteuliwa wa kaunti, akiwemo Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja, wabunge na madiwani kutoka vyama vya United Democratic Alliance (UDA) na Orange Democratic Movement (ODM).
Katika hotuba yake, Rais alitangaza kuwa vifaa vilivyoonyeshwa katika uwanja wa Ikulu vitagawanywa kwa vikundi mara moja.
“Mwenyekiti wa kila kundi atatafuta wanachama wake na vifaa vyenu vitaingizwa kwenye magari kusafirishwa maeneo yenu. Nitashughulikia kila mmoja pia. Mtapokea kitu kupitia simu zenu,” alisema.
Viongozi waliokuwemo ni pamoja na Mbunge wa Makadara George Aladwa, Phelix Odiwuor wa Lang’ata, John Kiarie wa Dagoretti Kusini, Ronald Karuri wa Kasarani, Anthony Oluoch wa Mathare, Peter Orero wa Kibra, Mwenje Mark wa Embakasi Magharibi, Seneta Tabitha Mtinda, Beatrice Elachi wa Dagoretti Kaskazini, Seneta Karen Nyamu, T.J Kajwang wa Ruaraka, Tim Wanyonyi wa Westlands, Esther Passaris, pamoja na madiwani kadhaa.
Mbunge Aladwa alisema kuwa wanaopinga serikali jumuishi wataondolewa mwaka 2027.
“Ninasikia viongozi wengine wakizungumza dhidi ya serikali hii jumuishi. Nataka kuwahakikishia kuwa chama cha ODM kiko ndani ya serikali jumuishi na tunamuunga Rais mkono. Wale wanaopingana na serikali hii wana uhuru wa kuondoka,” alisema Aladwa.
Mbunge huyo pia aliwahakikishia baadhi ya madiwani wa ODM wa Bunge la Kaunti ya Nairobi kwamba hawafai kuogopa mtu yeyote.
Diwani wa Makongeni, ambaye pia ni Kiongozi wa Wengi Bungeni Peter Imwatok, hakuhudhuria hafla hiyo pamoja na Kiongozi wa Wengi Msaidizi Moses Nyangaresi Ogeto anayewakilisha wadi ya Kilimani.
Madiwani wengi wa ODM hawakuhudhuria hafla hiyo. Kwa mujibu wa taarifa iliyopatikana na Taifa Leo, Imwatok alisema kuwa wanachama wote wa Azimio hawakufurahishwa na maandalizi yake.