Habari za Kitaifa

Mtahiniwa azirai baada ya kupigwa na afisa wa elimu

Na  WYCLIFFE NYABERI November 13th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

MSICHANA mtahiniwa wa mtihani wa Kidato cha Nne (KCSE) katika Shule ya Wasichana ya Sironga, Kaunti ya Nyamira alikimbizwa hospitalini mnamo Jumanne, Novemba 12, 2024 baada ya kuzabwa makofi na afisa wa Wizara ya Elimu.

Afisa huyo anayesimamia ubora wa elimu, anasemekana kuzuru shule hiyo ya kitaifa Jumanne asubuhi ili kukagua jinsi mtihani huo ulikuwa unaendelea.

Alipoingia kwenye chumba kimoja cha mtihani, aliona mtahiniwa mmoja akitafuna kitu ambacho alishuku kuwa ni “Mwakenya.”

Mwakenya ni kijikaratasi kidogo ambacho wanaodanganya katika mitihani huandika majibu ya maswali wanayotarajia yatakuwa kwenye mtihani. Ikiwa majibu ya swali lililoulizwa liko kwenye Mwakenya huo, basi watahiniwa hao hugeukia kijikaratasi hicho ili kiwe msaada kwao.

Kulingana na ripoti ya polisi, afisa huyo alipoona hayo, alisogea alikokuwa mtahiniwa huyo na kuanza kumzaba makofi mazito mazito na kisha akaondoka shuleni.

Kufuatia kipigo hicha, mtahiniwa huyo alizongwa na mawazo alipokuwa akifanya karatasi yake ya asubuhi.

Lakini muda wa mtihani wa karatasi hiyo ulipokaribia kwisha, mtahiniwa huyo alianguka kwenye chumba cha mtihani.

Alikimbizwa katika zahanati ya shule, ambapo hali yake iliimarika

Polisi wameanza uchunguzi kuhusu suala hilo.

“Uchunguzi wa tukio hilo umeanza na maelezo zaidi yatafuata,” ilisema sehemu ya ripoti ya polisi.

Takriban miezi miwili iliyopita, shule hiyo ya pekee ya kitaifa ya wasichana huko Nyamira, ilipatwa na msiba baada ya mwanafunzi wa kidato cha nne kufariki kwa kujitoa uhai.

Mwanafunzi huyo aliruka kutoka orofa ya tatu ya jengo la usimamizi wa shule majira ya alfajiri wikendi moja wenzake walipokuwa wakijiandaa kuanza siku.

Marehemu hakuacha maelezo yoyote kuhusu kwa nini alijitoa uhai.