Habari za Kitaifa

Mtanizoea, sibanduki ofisini na sitafutwa, Duale achemkia wabunge

Na SHABAN MAKOKHA September 4th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WAZIRI  wa Afya, Adan Duale, amesema hatajiuzulu kuhusiana na sakata katika Bima ya Afya ya Jamii (SHA), akisisitiza kuwa hana hatia yoyote katika ukora ambao unaendelea kufichuliwa. 

Bw Duale pia amewapuuza wanasiasa wanaotaka afutwe kazi, akisema hawana misingi ya kikatiba ya kumtimua.

“Sababu za kumtimua Waziri zimeainishwa wazi katika Katiba, na mimi sijakiuka yoyote. Nimeziba mianya waliyokuwa wakitumia kuiba mali ya umma, na sasa wamekasirika, lakini hatutatishwa,” alisema Bw Duale.

Kauli hiyo ilitolewa huku kukiwa na shinikizo kutoka kwa viongozi wa upinzani wanaomhusisha na kashfa ya SHA.

Mapema wiki hii, wabunge wa Muungano mpya wa Kenya Moja walimtaka Bw Duale ajiuzulu kwa madai ya kuhusika na ufisadi katika SHA.

“Pale palipo na pesa, matapeli hufuata. Vituo vya afya vimekuwa vikishirikiana na magenge ya wizi kuwapora wagonjwa kupitia mfumo wa kidijitali wa Afya, ambapo watumiaji wanaweza kufuatilia taarifa zao, magenge haya hayana nafasi tena ya kujitajirisha kupitia wagonjwa,” akaongeza waziri huyo.

Akiwa Kakamega, Bw Duale alikanusha kumiliki kampuni yoyote inayotoa huduma kwa SHA, na kuwataka wanasiasa wanaomshutumu, wakiongozwa na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna, watoe ushahidi wa madai yao.

“Niko tayari kufika mbele ya chombo chochote cha uchunguzi ili kueleza na kutetea mali yangu yote,” alisema, huku akisisitiza kuwa amejitolea kuleta mageuzi katika sekta ya afya nchini.

Bw Duale alitangaza kuwa serikali iko mbioni kulipa madeni yote yaliyokuwa yakidaiwa na watu binafsi na watoa huduma za afya chini ya mpango uliokuwepo wa Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Afya (NHIF) ambapo jumla ya Sh30 bilioni  zimetengwa kulipa madeni hayo.

Akizungumza alipokuwa akizindua mradi wa Taifa-Care katika Kaunti ya Kakamega, Waziri Duale alisema jumla ya Sh5.3 bilioni zinadaiwa na watu binafsi, huku asilimia 92 ya madeni yote ya NHIF yakiwa chini ya Sh10 milioni.

“Tunasubiri Wizara ya Fedha kuwasilisha bajeti ya ziada ili Wizara ya Afya ipate fedha zinazohitajika kulipa madeni haya,” alisema Bw Duale.

Alieleza kuwa madeni ya zaidi ya Sh10 milioni yatapitiwa upya na kikosi kilichoteuliwa  na Wizara ya Afya kabla ya malipo kuidhinishwa.

Gavana wa Kakamega, Fernandes Barasa, alithibitisha kuwa hospitali katika kaunti hiyo tayari zimeanza kupokea fedha kutoka SHA.

Hata hivyo, alitoa wito kwa wizara hiyo kuharakisha mchakato huo ili huduma za afya zisiathirike

“Kaunti ya Kakamega ina zaidi ya watu milioni 1.9, na tayari tumesajili zaidi ya Sh800 milioni kupitia SHA. Lakini tuna madeni ya Sh293  milioni ambayo ni muhimu kulipwa haraka,” akasema Bw Barasa.