Mtego wa Ruto ulivyomnasa Rigathi eneo la Mlima Kenya
HUKU mdahalo kuhusu mpango wa kumtimua ofisini Naibu Rais Rigathi Gachagua ukishika kasi, wadadisi wa masuala ya kisiasa sasa wanasema huenda aliwekewa mtego kwa kutwikwa jukumu la kuongoza mageuzi ya sekta ndogo ya kahawa na chai.
Sekta hizo ndizo uti wa mgongo wa kiuchumi wa eneo la Mlima Kenya na kushindwa kwake kuzirekebisha kungemfanya akosane na wakazi wa ngome yake ya kisiasa.
Punde tu Rais William Ruto alipomteua kusimamia mageuzi katika sekta hiyo, Naibu Rais alisema kuwa serikali haingeruhusu vitisho kutoka kwa kampuni na mabroka ambao alisema wamewafyonza wakulima wa kahawa kwa muda mrefu sana.
Alisema hali ilivyokuwa katika sekta hizo ilisababishia wakulima “kila aina ya mateso” na akaahidi kuyashughulikia kwa manufaa ya wakulima.
Hata hivyo, chini ya mwaka mmoja baada ya kuapa kuangamiza makundi hayo, Naibu Rais alianza kulia akisema makundi hayo yalikuwa yakimpiga vita na akaomba Mungu amsaidie kuyashinda.
“Tumeshindwa, si kwa sababu sisi ni wavivu au kwa sababu tumeshindwa kufanya kazi bali kwa sababu mitandao ya mabroka imekita mizizi sana. Kuna takriban vikundi vitatu hadi vinne ambavyo vimepangwa vyema,” aliambia mkutano katika Kanisa la Kagere PCEA Othaya, Kaunti ya Nyeri.
Alisema kwamba vita ya kufufua sekta hiyo havikuwa vya watu wenye mioyo dhaifu na akaahidi kuendelea navyo.
Bw Herman Manyora, mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi anasema aina ya mageuzi yanayotarajiwa katika sekta hizo ni makubwa sana hivi kwamba mtu hawezi kufaulu kuyafanikisha peke yake.
Alisema katika kipindi cha miaka 60 tangu uhuru, sekta za kahawa na chai zinadhibitiwa na mitandao ya mabroka kote duniani na kuivunja hakuwezi kuwa kazi ya mtu mmoja.
“Sekta hizi kwa miaka mingi zimekuwa mikononi mwa watu na mashirika ambayo yanalindwa na watu wakubwa na wenye nguvu, na ni biashara za kimataifa na si rahisi kukabiliana nazo,” Bw Manyora alisema katika mahojiano ya simu.
Alisema baadhi ya majukumu yanahitaji nia njema kutoka pande zote, na ikikosa inatatatiza matokeo yanayotarajiwa, akiongeza kuwa huenda Bw Gachagua alijikuta katika hali hii alipoanza kulia kwamba mabroka hao walikuwa na “nguvu nyingi”.
Baadhi ya wadau katika sekta ya kahawa hata hivyo wanasema Bw Gachagua amepata mafanikio fulani, huku mwenyekiti wa Muungano wa Wazalishaji Kahawa Kaunti ya Meru Bw Zablon Mbaabu akitaja kuanzishwa kwa Mfumo wa Malipo wa Moja kwa Moja(DSS) kama ushindi kwa wakulima.
Kupitia DSS, benki zilizoteuliwa hulipa wakulima moja kwa moja bila hitaji la kupitia maajenti.
Lakini matukio ya hivi majuzi katika eneo lote la Mlima Kenya yanaonyesha kuwa mageuzi yanayotarajiwa katika sekta ndogo ya chai na kahawa yamefeli.
Wakulima waliokata tamaa wamekuwa wakifanya maandamano wakilalamikia kupungua kwa malipo ya mazao hayo.
Mnamo Septemba 9, 2024 siasa za Mlima Kenya zilijitokeza wakati wa mkutano wa wakulima wa kahawa ulioongozwa na Waziri wa Vyama vya Ushirika Wycliffe Oparanya huko Karatina ambapo viongozi wa eneo hilo walimshambulia Gachagua wakimsawiri kama aliyeshindwa kufufua sekta ndogo.
Taharuki ilitanda katika mkutano maalum wa chama cha wakulima wa kahawa cha Baricho uliogeuzwa kuwa mapambano ya kisiasa huku wanasiasa watatu wa eneo hilo wakisema Bw Gachagua alikuwa ameshindwa kusaidia wakulima.
Bw Oparanya ambaye aliongoza mkutano huo alisema aliagizwa na rais kuuitisha kufuatia kilio cha wakulima wa chama kilichokumbwa na madeni ambapo rais alijitolea kulipa takriban Sh63 milioni ambazo zilidaiwa ‘kuibiwa’ na baadhi ya maafisa wa usimamizi.
Waziri alikiri jukumu la Bw Gachagua akisema tu “ninaelewa kuwa naibu rais anatoka eneo hilo. Nasikia siasa hapa ni moto na najua wote mnamuunga mkono rais. Naibu rais anatoka hapa lakini kwa vile amekuwa kimya, nimetumwa na rais ambaye ameskia kilio chenu,” Bw Oparanya alisema.
Rais Ruto alimtuma Mbunge wa Mathira Eric Wamumbi kuwasilisha “habari njema” kwa wakulima hao wa kahawa.
Bw Wamumbi, mwenzake wa Nyeri mjini, Bw Duncan Maina na Seneta wa Nyeri Wahome Wamatinga hawakutaja wala kutambua jukumu la Bw Gachagua katika kurekebisha sekta hiyo.
Bw Wamumbi, ambaye alimrithi Bw Gachagua kama mbunge wa Mathira ni mshirika wa zamani wa naibu rais ambaye aligeuka kuwa adui na sasa ndiye mkosoaji wake mkubwa, alisema “alizungumza moja kwa moja” na Rais Ruto ambaye aliahidi kuwaokoa wakulima.