Mtulipe pesa zetu tuondoke, wanajopo wa IEBC wasema
NA CHARLES WASONGA
WANACHAMA wa jopo la kuteua makamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) sasa wanataka walipwe kwa muda waliohudumu kabla ya kazi yao kusimamishwa.
Kwenye memoranda waliowasilisha bungeni, wanachama wa jopo hilo wakiongozwa na mwenyekiti wao Nelson Makanda pia wanataka wadumishwe katika jopo jipya litakaloteuliwa baada ya kupitishwa kwa Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya IEBC unaojadiliwa wakati huu bungeni.
“Wanachama wote wa jopo la kuteua makamishna wa IEBC watakaoondoka baada ya mswada huu kuwa sheria sharti walipwe kwa kazi waliofanya,” Dkt Makanda anasema kwenye memoranda hiyo iliyowasilishwa kwa Kamati ya Pamoja ya Bunge la Kitaifa na Seneti kuhusu Haki na Masuala ya Kikatiba (JLAC).
Anataka kamati hiyo inayoongozwa kwa pamoja na Mbunge wa Tharaka George Murugara na Seneta wa Bomet Hillary Sigei ipendekeze walipwe kuanzia wakati ambapo waliapishwa hadi wakati ambapo jopo hilo litavunjwa rasmi kulingana na sheria iliyolibuni.
Wanachama wengine wa jopo hilo ni Charity S. Kisotu (Naibu Mwenyekiti), Bethuel Sugut, Novince Euralia Atieno, Evans Misati James, Benson Ngugi Njeri na Fatuma Saman.
Kulingana na mwongozo wa malipo uliotolewa na Tume ya Kukadiria Mishahara na Marupurupu wa Watumishi wa Umma (SRC), kuhusu malipo ya wanachama wa majopo teule, mwenyekiti wa jopo hilo anafaa kulipwa marupurupu ya Sh30,000 kila siku akiwa afisini.
Nao wanachama wengine sita wanapaswa kutia kibindoni Sh25,000 kila siku. Jopo hilo pia lina katibu ambaye anastahili kulipwa Sh20,000 kwa kila kikao, mkuu wa kitengo cha ufundi hulipwa Sh10,000 kwa kila kikao huku makarani na walinzi wakilipwa Sh4,000 kwa kila kikao.
Kwa hivyo, endapo ombi la Dkt Makanda litakubaliwa, haijulikani kiasi cha fedha ambazo wanachama wa jopo hilo watalipwa.
Jopo la Dkt Makanda liliteuliwa mnamo Februari 27, 2023, na Rais William Ruto ambapo majina yao yalichapishwa kwenye gazeti rasmi la serikali.
Jopo hilo lilianza kutekeleza majukumu yake mnamo Machi 2, 2023, baada ya Dkt Makanda na wenzake kuapishwa rasmi na Jaji Mkuu Martha Koome.
Kufikia Aprili 27, 2023, wakati jopo hilo liliagizwa kusitisha shughuli zake kwa muda kutoa nafasi kwa Kamati ya Kitaifa kuhusu Mazungumzo (Nadco) katika ukumbi wa Bomas of Kenya, lilikuwa limepokea maombi kutoka kwa watu kadhaa waliotaka kushindania wadhifa wa mwenyekiti na makamishna wa IEBC.
Kulingana na takwimu za muda zilizotolewa na Dkt Makanda, jopo hilo lilikuwa limepokea majina ya watu 25 waliotaka kujaza nafasi ya mwenyekiti huku wengine 925 wakipania kushindania nafasi sita za makamishna wa IEBC.
Kulingana mswada mpya wa marekebisho ya sheria ya IEBC unaojadiliwa bungeni wakati huu, idadi ya wanachama wa jopo la kuteua makamishna wa tume hiyo imeongezwa kutoka saba hadi tisa.