Mudavadi aongezewa majukumu serikalini, Gachagua akilumbana na wanasiasa Mlimani
IMANI ya Rais William Ruto kwa Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi inaendelea kudhihirika baada ya hatua yake ya kumtwika majukumu zaidi ya kiserikali.
Rais Ruto anaonekana kumwamini sana Bw Mudavadi kutekeleza ajenda za serikali yake hasa mabadiliko ya kiuchumi na mashauri ya nje, wadhifa aliomtwika alipomteua Waziri wa Mashauri ya Kigeni mwaka jana.
Rais Ruto alimteua kuwa Waziri wa Mashauri ya Kigeni na Masuala ya Wakenya wanaoishi ng’ambo katika mabadiliko ya kwanza aliyofanyia baraza la mawaziri.
Imeibuka kuwa kiongozi wa nchi sasa ameweka wizara tano muhimu chini ya Bw Mudavadi katika kile wadadisi wanasema ni kutia muhuri imani aliyo nayo kwa naibu waziri mkuu huyo wa zamani na kutuma ujumbe fulani wa kisiasa.
Mbali na Wizara ya Mashauri ya Kigeni na Masuala ya Wakenya wanaoishi Ng’ambo, Bw Mudavadi atashirikisha wizara za Leba, Hazina Kuu (Fedha), Uwekezaji, Biashara na Kilimo katika juhudi za Rais William Ruto kufufua uchumi wa taifa.
Hatua hii inaweka mawaziri Florence Bore (Leba), Njuguna Ndung’u (Hazina Kuu), Rebecca Miano (Biashara) na Mithika Linturi (Kilimo) chini ya Bw Mudavadi katika mkakati wa Rais Ruto wa kuimarisha ushirikiano wa Kenya kidiplomasia na kiuchumi.
Kulingana na Amri ya Rais nambari 2 ya 2023, Dkt Ruto alieleza kuwa Bw Mudavadi “kwa ushirikiano na Wizara ya Leba na Ulinzi wa Jamii” ataongoza utekelezaji wa Sera ya ajira Kimataifa,” kama nguzo kuu ya sera ya Kenya kuhusu mahusiano ya kigeni.
Alisema afisi ya Bw Mudavadi itafanya kazi “kwa ushirikiano na Waziri wa Hazina Kuu, Uwekezaji, Bishara na Viwanda, Kilimo na wizara nyinginezo katika sekta ya uzalishaji kuimarisha ushirikiano wa Kenya kidiplomasia na kiuchumi.
Wadadisi wanasema Dkt Ruto anamwamini Bw Mudavadi kwa kuwa ndiye mwanachama wa Baraza lake la Mawaziri mwenye tajiriba pana na asiyependa kuchangamkia siasa akilinganishwa na Naibu Rais Rigathi Gachagua.
“Mudavadi ndiye waziri mwenye uzoefu mkubwa mbali na kuwa wadhifa wake wa mkuu wa mawaziri unaweka wenzake chini yake. Pili, sio mwepesi wa makabiliano ya kisiasa kama baadhi ya wenzake katika baraza la mawaziri akiwemo Naibu Rais Rigathi Gachagua,” asema mchambuzi wa siasa Dkt Isaac Gichuki.
Ingawa wadhifa wake ni wa kuteuliwa ikilinganishwa na wa Bw Gachagua ambao alichaguliwa akiwa mgombea mwenza wa Dkt Ruto, kumekuwa na vita vya ubabe kati ya viongozi hao wawili wakiwania kuvutia imani ya kiongozi wa nchi.
Dkt Gichuki anasema kuna dalili kuwa Dkt Ruto anamwandaa Bw Mudavadi kutekeleza jukumu kubwa zaidi la kisiasa.
“Kwa kumtwika majukumu haya huku akimuacha Bw Gachagua, ujumbe wa kisiasa unaoibuka ni kwamba mbunge huyo wa zamani wa Sabatia atakuwa nguzo katika mipango ya kisiasa ya Rais,” alisema.
Mwaka jana, Seneta wa Kakamega Boni Khalwale alidai kuwa Rais Ruto aliwadokezea viongozi wa eneo la Magharibi kwamba ataunga kiongozi kutoka jamii ya Mulembe kumrithi atakapokamilisha muhula wa pili mwaka wa 2032, kauli iliyochukuliwa kuwa anamwandaa Bw Mudavadi kuingia ikulu badala ya Bw Gachagua.
Huku Bw Gachagua akilumbana na wanasiasa wengine wa eneo la Mlima Kenya kuhusu siasa za uchaguzi wa 2027 na 2032, Bw Mudavadi anaendelea kutwikwa majukumu zaidi.
Mchambuzi wa siasa, David Rono anasema kinachomfanya Mudavadi kuwa kipenzi cha Ruto ni hulka yake ya utiifu, unyenyekevu na uzoefu wa miaka mingi serikalini.
“Katika siasa, anatoka eneo lililo na kura nyingi ambalo Rais Ruto anaweza kutegemea iwapo Mlima Kenya utamuasi katika uchaguzi mkuu wa 2027,” aeleza Dkt Rono.