Mungatana apinga sera ya ‘mtu-mmoja, kura moja, shilingi moja’ anayoshabikia Gachagua
NA CHARLES WASONGA
SENETA wa Tana River Danson Mungatana ameshutumu Naibu Rais Rigathi Gachagua kwa kuunga mkono pendekezo kwamba ugavi wa mapato ya serikali katika maeneo mbalimbali nchini ufanywe kwa msingi wa idadi ya watu.
Akiwahutubia wanahabari katika Majengo ya Bunge mnamo Jumatano, Bw Mungatana alisema wao kama viongozi kutoka maeneo kame (ASAL) nchini wanapinga vikali sera hyo kwani itayatenga kimaendeleo hata zaidi.
“Tungetaka kumwambia Naibu Rais kwamba sisi viongozi kutoka maneo kame nchini tunaunga mkono mfumo wa ugavi wa mapato kwa msingi wa ukubwa wa eneo yaani ‘one -man, one-vote, one-kilometre’. Lakini tunapinga vikali huu mfumo anaoupigia debe wa, ‘one-man, one-vote, one-shilling’,” Bw Mungatana akasema.
Seneta huyo aliyechaguliwa kwa tiketi ya chama cha United Democratic Alliance (UDA) alidai sera hiyo inayoshabikiwa na Bw Gachagua inarejesha Kenya katika enzi za sera ya maendeleo iliyoasisiwa na aliyekuwa Waziri wa Mipango ya Kiuchumi Tom Mboya ambayo ilitenga maeneo kame kimaendeleo.
“Huu mfumo wa ugavi wa rasilimali unaopendekezwa na Bw Gachagua umepitwa na wakati na ni kinyume cha Katiba ya sasa inayoendeleza usawa kwa Wakenya wote pasina kuzingatia maeneo wanakotoka. Namwambia Bw Gachagua kwamba huu mfumo unaturejesha katika sera potovu iliyopendekezwa na marehemu Mboya wakati wa uhai wake alipopendekeza taarifa ya maendeleo nambari 10 ya 1965,” Bw Mungatana akaeleza huku akieleza kuwa kauli yake inawakilisha msimamo wa viongozi kutoka kaunti za Isiolo, Turkana, Marsabit, Mandera, Lamu miongoni mwa kaunti nyingine.
Akiongea Jumapili katika Kaunti ya Embu, Bw Gachagua alisema kuwa ataunga mkono mfumo wa ugavi wa mapato kwa msingi wa idadi ya watu ili kufikia kile alichodai kuwa ni usawa na haki katika kaunti.
“Katika ugavi wa mapato, naunga mkono mfumo wa mtu-mmoja, kura-moja, shilingi-moja. Rasilimali zinahusu watu. Mkiwa wengi inamaanisha kuwa mwalipa kiasi kikubwa cha ushuru. Kwa hivyo, ni wazi kwamba mnapolipa kiasi kikubwa cha ushuru, mwapaswa kupata sehemu kubwa ya mgao wa mapato kutokana na ushuru huo,” akasema Bw Gachagua.
Bw Gachagua alisema hayo alipohudhuria sherehe ya kutawazwa kwa Naibu Askofu Dkt John Kimani Nthiga katika Kanisa la Anglikana la St Peters katika mji wa Siakago, Kaunti ya Embu.
Lakini Jumatano Bw Mungatana alidai kuwa kauli ya Bw Gachagua inaakisi msimamo wake kama mtu binafsi wala sio msimamo wa serikali ya muungano tawala wa Kenya Kwanza.
“Baraza la mawaziri halijaketi kuidhinisha sera kama hii. Na mkutano wa kundi la wabunge wa Kenya Kwanza au chama chetu cha UDA haujaitishwa na kupitisha sera mbaya kama hiyo. Kwa hivyo, tujuavyo ni kwamba huo ni msimamo wa Gachagua kama mtu binafsi,” seneta huyo akaeleza.