Habari za Kitaifa

Murkomen aunga mkono polisi kuomba raia pesa za mafuta ya gari wakiripoti uhalifu

Na  GEORGE ODIWUOR September 18th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WAZIRI wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen amewatetea maafisa wa polisi ambao wanaomba ‘mafuta’ kutoka kwa Wakenya kabla ya kuwasaidia wakati wa dharura.

Bw Murkomen alisema kuwa polisi hawatekelezi kosa lolote wakiomba pesa za kununua mafuta kutoka kwa Wakenya kwa sababu mafuta huwa yanaisha na hawana njia nyingine ya kuyapata.

“Tusidanganyane kuhusu suala hili. Polisi huomba pesa ya mafuta kwa sababu ya mpango wetu wa kukodi ambapo wao hutengewa mafuta ya kiwango fulani kwa kila gari. Yakiish hawana namna nyingine,” akasema Bw Murkomen.

Chini ya mpango huo kila gari la polisi hupokea lita 450 za petroli au dizeli kwa kila mwezi. Kwa mujibu wa Bw Murkomen, mafuta hayo huisha chini ya wiki tatu.

“Baadhi ya magari hayo huwa yanaisha mafuta ndani ya siku 18 wakati maafisa wetu wanaendesha oparesheni ikiwemo kuwapeleka mahabusu kortini kisha kuwarejesha kwenye gereza,” akaongeza.

“Polisi wakiwaambia Wakenya magari yao hayana mafuta huwa wanafikiria polisi hao wanawaitisha hongo. Huo si ukweli,” akasema.

Alifafanua kuwa wakati mwingine, makamanda wa polisi wa vituo mbalimbali hukosa mafuta na hilo hufanya iwe vigumu kuendelea kwao na oparesheni au shughuli za kudumisha usalama.

Waziri huyo alikuwa akiongea wakati wa kikao cha Jukwaa la Usalama katika Kaunti ya Homa Bay. Alisema kati ya sababu ambazo zinafanya mafuta yanayotengewa magari ya polisi yaishe haraka ni umbali mrefu kutoka kituo cha polisi hadi kituo cha mafuta.

“Kufikia wakati ambapo wanarudi na kuanzisha oparesheni, mafuta hayo yatakuwa yameisha. Kwa muda ambao umesalia gari hilo litakuwa limeegeshwa kituoni likisubiri mwezi mwingine ili lijazwe mafuta,” akasema.

Ingawa hivyo, alisema wizara yake imeweka mikakati na mipango ya kushughulikia suala hilo.Alisema Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja anashughulikia mipango ya kuangazia na kuongeza kiwango cha mafuta ambayo magari ya polisi hutengewa.Waziri huyo alisema magari ya polisi sasa yatatengewa lita 650 za petroli au dizeli kila mwezi, ambalo ni ongezeko la lita 200.

Kisha vituo vipya vya mafuta vitajengwa kupunguza safari za magari ya polisi hasa katika kaunti kubwa na pana. “Tunalenga kupunguza kilomita kutoka kituo cha polisi hadi kituo cha mafuta hasa kwenye kaunti pana,” akasema Bw Murkomen.

Kauli ya waziri huyo ilizua maoni mseto huku baadhi ya raia wakikashifu polisi kwa kutumia mafuta ya magari yao kwa shughuli zao za kibinafsi.

“Magari ya serikali huwa yanastahili yatumike kuwasaidia Wakenya. Polisi wengine huyatumia magari hayo kwa biashara zao za kibinafsi kisha mafuta yakiisha, wao huwaomba Wakenya,” akasema Mwenyekiti wa Bunge la Wenyenchi Homa Bay Walter Opiyo.

Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Waislamu nchini (SUPKEM), utanzu wa Homa Bay Nuhu Masoud alisema hakuna utata wowote iwapo polisi watasaidiwa kwa kupewa mafuta.

“Huwa hawaulizi wasaidiwe lakini wanahitaji. Ufisadi katika idara ya polisi ni dhana tu ambayo Wakenya wamebuni,” akasema Bw Masoud.

Wakati wa jukwaa hilo la usalama polisi, maafisa wa utawala wa kieneo na kitaifa walikuwa na nafasi ya kujadili masuala yanayowaathiri wakati wa utendakazi wao na kuomba yapate suluhu.

Baadhi walisema wanafanya kazi katika afisi zilizochakaa huku wengine wakiomba magari ili wayatumie kuendeleza kazi zao.Bw Murkomen alisema serikali ipo katika harakati ya kuanzisha zabuni ya kununua magari ya usalama.

“Najua maafisa wengi wanajinyima na wengine wanavuka visiwa ambako wao hutumia rasilimali nyingi. Nataka Inspekta Jenerali wa polisi atambue hilo na kulishughulikia katika bajeti ya utawala,” akasema Bw Murkomen.