Mvua kuendelea kushuhudiwa maeneo mengi nchini – Utabiri
NA CHARLES WASONGA
IDARA ya Utabiri wa Hali ya Anga imetangaza kuwa sehemu nyingi nchini zitashuhudia mvua kubwa ndani ya siku saba zijazo.
Sehemu za kusini mwa Kenya zitashuhudia mvua kubwa ilhali sehemu za Kaskazini Mashariki na Kaskazini Magharibi zitaendelea kuwa kavu.
“Kuanzia Jumamosi hadi Januari 12, 2024, mvua zinazoandamana na ngurumo za radi zitashuhudiwa eneo la Kusini mwa Bonde la Ufa na nyanda za chini za Kusini Mashariki. Lakini maeneo ya Kaskazini Mashariki yatasalia kuwa kavu,” ikasema taarifa kutoka idara hiyo iliyotolewa Ijumaa.
Utabiri huo umejiri wakati ambapo mvua kubwa ilishuhudiwa Nairobi na sehemu kadhaa nchini.
Aidha, utabiri huo unaonyesha kuwa nyanda za juu mashariki mwa Bonde la Ufa na Kati mwa Kenya yatashuhudia mvua katikati mwa Januari.
Kulingana na kituo cha utabiri wa hali ya anga cha Shirika la Maendeleo la Igad, sehemu kubwa za Upembe wa Afrika zinatarajia kupokea mvua kubwa kati ya Januari na Machi 2024.