• Nairobi
  • Last Updated May 22nd, 2024 5:47 AM
Mvulana aliyejichomoa msituni Shakahola kuendelea na masomo aomba ufadhili

Mvulana aliyejichomoa msituni Shakahola kuendelea na masomo aomba ufadhili

NA ALEX KALAMA

MVULANA Issa Ali aliyefanya Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Nane (KCPE 2023) na kupata alama 259 kutoka Shule ya Msingi ya St Andrews mjini Malindi, anaomba ufadhili kujiunga na Kidato cha Kwanza katika Shule ya Upili ya Barani.

Shangazi yake, Bi Teresa Kanazi, alisema Jumamosi kwamba kijana huyo ni mmoja wa watu waliofanikiwa kujichomoa kutoka msituni Shakahola ambako mauaji ya zaidi ya watu 400 yanayohusishwa na mafundisho potovu ya kidini, yalifanyika.

Bi Kanazi alisema babake kijana huyo aliaga dunia mapema na mamake akaamua kujiunga na Kanisa la Good News International la mhubiri Paul Mackenzie. Familia hiyo ilikuwa ni ya imani ya Kiislamu.

Ali alisema alipoona hafaidiki na chochote msituni, alitafuta mbinu ya kujichomoa ili kukata kiu ya elimu na kujitafutia mustakabali bora maishani.

Alisema akiwa msituni, aliwasiliana na shangazi yake kwa kujiiba asionekane na viongozi wakuu waliosimamia masuala ya kiroho mle msituni. Alifanya hivyo kwa kutumia simu za baadhi ya wahudumu wa bodaboda ambao mara moja moja walifika mle msituni kupeleka ama maji au chochote kingine walichopewa kufikisha huko.

Bado familia inasubiri majibu ya vipimo vya vinasaba vya DNA ili ifahamike ikiwa mwili wa mamake Ali, ni miongoni mwa ile iliyoondolewa kwenye makaburi yaliyofukuliwa msituni.

Akizungumza na wanahabari mjini Malindi, Ali alisema hali ilivyo ikisalia kuwa hivyo, atakosa kuendelea na masomo yake kutokana na kukosa fedha za kulipia karo yake ya shule.

“Nilifanya KCPE mwaka 2023 na nimeitwa kujiunga na Shule ya Barani ila hatuna pesa za karo,” akasema mvulana huyo.

Kutokana na hali hiyo, Ali amewataka wadau, mashirika, viongozi na hata serikali kujitokeza na kumlipia karo ili apate kujiunga na shule ya upili na kuendeleza masomo yake ili kutimiza ndoto zake maishani.

Ali mwenye umri wa miaka 17 alikosa kuendelea na masomo yake kwa muda, baada ya kuwa mfuasi wa kanisa la Good news International, na hatimaye kujiondoa katika kanisa hilo mwaka 2020 na kisha kuendelea na masomo yake.

Kulingana na shangazi yake ni kwamba mamake Ali aliendelea kumfuata mhubiri Mackenzie huko Shakahola.

Bi Kanazi alisema zipo familia ambazo zimeshafahamishwa matokeo ya vipimo vya vinasaba vya DNA kutambua miili ya wapendwa wao walioangamia msituni Shakahola.

Lakini wao wameambiwa wawe na subira.

“Familia zinafahamishwa matokeo hayo ya DNA kupitia simu. Sisi tuliambiwa tusubiri hadi wiki ijayo ambapo ndipo huenda tukapewa matokeo,” akasema Bi Kanazi.

Kufikia Ijumaa, wataalamu wa DNA walikuwa wamefanikiwa kutambua miili 40 na kufahamisha familia za waliopoteza wapendwa wao. Miili hiyo ni sehemu tu ya jumla ya miili 429 iliyofukuliwa kwenye makaburi msituni Shakahola.

Upasuaji na uhifadhi wa miili hiyo umekuwa ukifanyika katika mochari ya Hospitali Kuu ya Malindi.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Safari ya barobaro singo aliyeanza ufugaji na kuku 3, sasa...

Salah kukosa mechi ya Misri dhidi ya Cape Verde kwa sababu...

T L