Habari za Kitaifa

Mwakilishi wa Papa akana kanisa linaruhusu ndoa za mashoga

January 8th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

BENSON MATHEKA na KNA

MWAKILISHI wa Papa Mtakatifu nchini Kenya ambaye piani Askofu Mkuu wa Sudan Kusini Hubertus van Megen amesema kuwa kanisa katoliki halikubali ndoa za jinsia moja.

Alisema tamko la hivi majuzi la papa la kuwataka makasisi kubariki ndoa za jinsia moja halimaanishi kwa vyovyote vile kwamba kanisa linaidhinisha miungano hiyo bali lilikusudiwa kuleta watu hao karibu na Mungu na katika mchakato huo kuwasaidia kushinda dhambi zao.

Akizungumza katika kanisa kuu la Eldoret Sacred Heart alipoongoza hafla ya kutawazwa kwa makasisi wanane, Askofu mkuu Megen alisema baraka hizo zilikusudiwa watu binafsi lakini si baraka ya uhusiano  ambao alisema ni kinyume na mafundisho ya Kikristo.

Askofu Dominic Kimengich wa Dayosisi ya Katoliki ya Eldoret alisema kanisa linatambua kuwa ndoa ni kati ya mwanamume na mwanamke na kwa hivyo tamko la Papa Mtakatifu halifungui milango kwa njia yoyote kuidhinishwa kwa ndoa za jinsia moja.

Askofu Kimengich aliyeambatana na Askofu Mkuu wa Sudan Kusini, Hubertus van Megen, alisema kwa kweli katika mazingira ya Kiafrika, haitakiwi kuitwa baraka bali ni maombi kwa watu  wanaoishi katika ndoa hizo alizotaja kama dhambi kubadilika.

Mdahalo wa kuruhusu ndoa za jinsia moja, umezua hisia mseto wengi wa Wakenya wakipinga jambo hilo kutekelezwa nchini.

Wakati wa mahubiri yake, Askofu Megen alionya makasisi dhidi ya kujihusisha na wanasiasa akisema hii imesababisha kanisa kutumiwa na wanasiasa kwa maslahi yao ya binafsi.

Alisema viongozi wa dini wakiungana na wanasiasa  huwa wanapoteza uhuru wao kwa wanasiasa.

Kwa hiyo alitoa wito kwa makasisi wapya waliowekwa wakfu kumuiga Kristo na kujitahidi kusaidia maskini na waliokandamizwa.