• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 7:50 AM
Mwalimu azuiliwa kwa madai ya kukatakata na kuua mwanawe ‘aliyemjia kwa ubaya’

Mwalimu azuiliwa kwa madai ya kukatakata na kuua mwanawe ‘aliyemjia kwa ubaya’

Na ALEX NJERU

MWALIMU Mstaafu jana alidaiwa kumuua mwanawe kwa kumkata kwa panga katika Kaunti ya Tharaka-Nithi kufuatia mzozo wa pesa zilizopatikana baada ya kuuza ng’ombe.

Tukio hilo la kusikitisha lilifanyika katika kijiji cha Marichiu, Lokesheni ya Iruma eneobunge la Maara Jumanne, mwendo wa saa nne usiku.

Mzee Fabian Kaburu, 71 ambaye anaendelea kuzuiliwa na polisi akisubiri kushtakiwa, amedaiwa kumkata mwanawe Cliff Mwenda, 28 kichwani mara kadha. Bw Mwendwa alifariki papo hapo.

Mwana wa pili wa mzee huyo, Bw Maxwell Gitonga, 38 ambaye aliwasili hapo kujaribu kuwatenganisha wawili hao, naye amelazwa hospitalini akiwa na majeraha mabaya ya panga upande wa kushoto shingoni, kifuani na pia vidole vya mkono wa kushoto.

Baadhi ya watu wa familia na wanakijiji, walidai kuwa mwalimu huyo mstaafu amekuwa na tofauti kali na mwanawe ambaye amekuwa akimsumbua sana nyumbani.

Walidai kuwa marehemu amekuwa akimtaka babake amptie pesa huku wakati mwingine akiiba bidhaa za nyumbani na za majirani. Amekuwa akifanya hivyo ili kupata pesa za kununua pombe.

Siku ya tukio, Bw Mwenda alikuwa akitaka agawiwe pesa zilizotokana na kuuzwa kwa ng’ombe huyo wiki chache zilizopita.

Wanafamilia walisema kuwa marehemu amekuwa akimsumbua babake akitaka apokezwe mgao wake kwenye mauzo hayo.

Hata hivyo, babake amekuwa akimwaambia alitumia pesa hizo kutimizia familia yake mahitaji mbalimbali. Lakini alirejea mwisho wa mwezi wakati ambapo alijua babake alikuwa amepata malipo ya uzeeni.

Kulingana na jamaa zake, Bw Mwenda alimvamia babake kwa panga akiwa amelewa na kutaka pesa ndipo fujo hizo zikazuka.

Hapo ndipo nduguye Gitonga alifika kutaka kusaidia na kumnusuru babake ambaye alikuwa amelemewa na Mwenda na alikuwa hatarini.

Mambo yaliendelea kuwa mabaya baada ya Bw Gitonga, 38 naye kugeukiwa na marehemu ambaye alimkata kwa panga.

Kwa mujibu wa ripoti ya polisi, Mzee Kaburu kuona Gitonga aliyekuwa amekuja kumsaidia yupo hatarini, alitumia nguvu na kumpokonya Mwenda panga kisha akamkata kwa kichwa na kumuua papo hapo.

Mzee wa Kijiji Justus Mwitari alipiga ripoti kuhusu kisa hicho katika kituo cha polisi cha Magutuni na polisi wakafika kisha kubeba mwili wa Mwenda hadi chumba cha kuhifadhia maiti ya Hospitali ya Chuka Level Five.

Mzee kaburu alipatikana nyumbani ambapo alikamatwa na kupelekwa katika kituo cha polisi akisubiri kuwasilishiwa mashtaka katika Mahakama ya Chuka.

Mkazi, Bi Mary Kaari alisema kuwa marehemu alikuwa kero sana kwao kwa sababu alikuwa akiwaibia na kuvunja nyumba zao.

  • Tags

You can share this post!

Jamaa ashtuka demu aliyedhani mlokole ni mlevi

Kazi yenu ni kufinya kompyuta na kuweka pesa kwa mfuko,...

T L