Habari za Kitaifa

Mwanafunzi wa MMU aliuawa kwa kunyongwa

Na RICHARD MUNGUTI na KEVIN CHERUIYOT April 8th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MWANAPATHOLOJIA Mkuu wa Serikali Johansen Oduor amesema mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Multi-Media (MMU) Sylvia Kemunto aliuawa kwa kunyongwa.

Dkt Oduor aliyefanya upasuaji wa mwili wa Slyvia katika Mochari ya Montezuma, Nairobi alisema mwanafunzi huyo alinyongwa akijarbu kujiokoa.

“Baada ya kufanyia ukaguzi na upasuaji mwili wa Sylvia nimebaini kwamba kifo chake kilitokana na kunyongwa,” Dkt Oduor aliwaambia wanahabari katika Mochari ya Montezuma, Jumanne alasiri, Aprili 8, 2025.

Wakili wa familia ya Kemunto, Danstan Omari aliyeandamana na mama ya mwanafunzi huyo na watu wengine wa familia alisema “marehemu alijaribu kujiokoa na kupigana lakini akashindwa nguvu.”

Bw Omari alisema atashtaki MMU kwa kutolinda wanafunzi.

Wakili huyo alisema mshukiwa katika mauaji hayo ya Sylvia amezuiliwa kwa siku 21 kuwapa polisi muda kukamilisha uchunguzi.

Hakimu mwandamizi mahakama ya Kibra Zainab Abdul Jumatatu, Aprili 7 aliamuru Erick Mutinda Philip mwenye umri wa miaka 19 azuliwe katika kituo cha polisi cha Capitol Hill hadi Aprilii 28, 2025.

Bi Abdul alisema Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umama (DPP) Renson Ingonga ataamua ikiwa Mutinda atafunguliwa shtaka la mauaji ya mwanafunzi Kemunto.

Wote wawili Sylvia na Mutinda walikuwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Multi-Media.

Hakimu alikubalia ombi la afisa anayechunguza kesi hiyo kwamba anahitaji muda kukamilisha uchunguzi na kuandika taarifa za mashahidi.