Habari za Kitaifa

Mwanamume afa maji akisaidia kuvuta lori mtoni

May 11th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA GEORGE MUNENE

MWANAMUME mmoja amesombwa na maji ya mafuriko alipokuwa akisaidia kutoa lori la mchanga lililokuwa limetumbukia kwenye mto Ena uliovunja kingo zake kufuatia mvua kubwa katika Kaunti ya Embu.

Mwathiriwa huyo wa umri wa miaka 33 alikuwa miongoni mwa wanakijiji waliojitokeza katika daraja la Ena katika kijiji cha Kagaari kufanya uokozi alipokumbana na kifo chake.

Kulingana na walioshuhudia, mwathiriwa aliyetambulwa kuwa ni Moses Murimi almaarufu ‘Kanyama’, alikuwa akifunga kamba kwenye lori hilo kwa nia ya kulivuta akisaidiana na wanakijiji lakini akapigwa na mawimbi mazito ya maji ya mafuriko na kusombwa.

Wenzake pamoja na polisi walijaribu kumuokoa lakini juhudi zao hazikuzaa matunda.

Bado wanaendelea kutafuta mwili wa marehemu.

“Tulikuwa tukinasua lori wakati mwenzetu alisombwa na maji ya mto ambayo yameongeza kasi kufuatia mafuriko,” mwanakijiji mmoja aliambia Taifa Leo .

Lori hilo lilikuwa likielekea eneo la Runyenjes likiwa na watu watatu ambapo dereva alishindwa kulidhibiti na lilipofika kwa daraja, likatumbukia mtoni.

Hata hivyo watu watatu waliokuwa ndani ya lori wameokolewa na kupelekwa hospitalini kwa matibabu.