• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Mwanamume aishi na maiti ya dadake kusubiri afufuke

Mwanamume aishi na maiti ya dadake kusubiri afufuke

NA MERCY KOSKEI

MNAMO Jumatano, makachero kutoka Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) waliupata mwili wa mwanamke ukiwa umeoza vibaya katika nyumba moja katika eneo la YMCA jijini Nakuru.

Uchunguzi zaidi wa polisi ulibaini kuwa kifua cha mwanamke huyo kilikuwa kimefungwa kwa nakala ya Biblia.

Makazi hayo yanamilikiwa na Bw David Kinyanjui na mkewe, aliyemuoa majuzi.

Makazi hayo maridadi kwa mwonekano, sasa yamegeuka kuwa eneo la uhalifu linalochunguzwa na polisi. Kisa hicho kimezua msururu wa maswali.

Uchunguzi wa polisi umebaini kwamba kuna matukio yasiyoeleweka yaliyokuwa yakiendelea.

Mke wa David Kinyanjui. PICHA | BONIFACE MWANGI

Hali hiyo ilianza wakati dadake Bw Kinyanjui, Rosemary Wahu,60, aliwatembelea wanandoa hao Nakuru.

Kulingana na mwanawe  Wahu, Bw Boniface Mwangi, mamake alimtembelea mjombake Januari 15, 2024, baada ya kumwambia amemwoa mke mpya, miezi michache baada ya kutengana na mke wake.

Bw Kinyanjui alitaka wawili hao kujuana.

Bi Wahu aliondoka nyumbani kwake katika Kaunti ya Kiambu na kuelekea kwa nduguye, jijini Nakuru. Aliiambia familia yake kwamba alifika salama.

Bw Mungai alikuwa akiwasiliana na mamake hadi Januari 29, 2024, wakati mawasiliano yao kwa njia ya simu yalikatika katika hali tatanishi. Wakati alipojaribu kumuuliza mjombake, Bw Kinyanjui kuhusu yaliyomfika mamake, alianza kumpa maelezo mengi yasiyoeleweka.

“Kwa wakati mmoja, alisema simu yake ilianguka kimakosa kwenye maji na kuharibika,” akasema Bw Mungai, kwenye mahojiano na Taifa Leo.

Baada ya siku kadhaa za mvutano, Bw Mungai alisisitiza kwamba lazima azungumze na mamake, japo Bw Kinyanjui hakuwa akimruhusu, hali iliyozua maswali mengi.

Mnamo Jumanne, jirani mmoja wa Bw Kinyanjui alimwambia Bw Mungai kuhusu harufu mbaya iliyokuwa ikitoka kutoka kwa Bw Kinyanjui.

Jirani huyo pia alimwambia Bw Mungai kwamba mamake hakuwa ameonekana kwa zaidi ya wiki mbili, hali iliyozua hofu kwa jamaa za Bi Wahu.

Bw Mungai na jamaa zake waliamua kusafiri hadi Nakuru kutegua kitendawili cha alikokuwa mamake.

Walipoingia katika makazi ya Bw Mungai, waliupata mwili wa Bi Wahu ukiwa umeoza huku ukiwa umefungwa nakala ya Biblia kwenye kifua chake.

“Inaonekana kuna uwezekano alifariki wiki mbili zilizopita. Kuna harufu mbaya kote katika chumba hicho. Tunawaomba polisi kufanya uchunguzi wa haraka ili kubaini chanzo cha kifo hiki tatanishi,” akasema Bw Zack Wanjohi, ambaye ni jamaa wa marehemu.

Bi Penninah Wambui, ambaye ni jirani, alisema kuwa wanandoa hao wawili walisema harufu hiyo ilitokana na mzoga wa mbwa aliyekufa.

“Tuliambiwa walikuwa wakimngoja kufufuka. Hatujui kuhusu vile hilo lingefanyika. Huenda ni washirika wa kanisa la imani za giza,” akasema Bi Wambui.

Mkuu wa Polisi katika eneo la Nakuru Mashariki Mohamed Wako, alithibitisha kisa hicho, huku akieleza kuwa wameanza uchunguzi kubaini kiini cha kifo cha Bi Wahu.

Bw Mungai na mkewe wamekamatwa ili kuwasaidia polisi kufanya uchunguzi wao.

  • Tags

You can share this post!

Waziri Mkuu wa Haiti ‘ahepea’ Puerto Rico

Yalikuwa makosa kuunganisha polisi wa utawala na wa kawaida...

T L