• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 4:54 PM
Mwanamume aliyefaa kupelekwa Marekani kushtakiwa atoroka seli

Mwanamume aliyefaa kupelekwa Marekani kushtakiwa atoroka seli

NA MARY WANGARI

MASWALI yameibuka kuhusu jinsi mwanamume aliyekuwa akisubiri kukamilika mchakato wa kumpeleka nchini Marekani kushtakiwa alivyotoroka korokoroni katika hali ya kutatanisha mnamo Jumatano.

Adam Kevin Kinyanjui Kang’ethe alitoweka katika Kituo cha Polisi cha Muthaiga alimokuwa akizuiliwa baada ya ubalozi wa Marekani kuomba Kenya isaidie kumsafirisha hadi nchini humo kushtakiwa kwa kumuua mpenzi wake na kisha kuutupa mwili wake kwenye uwanja wa ndege.

Duru za polisi zinaashiria kuwa mshukiwa alitoweka kituo hicho mwendo wa kumi na moja punde baada ya kukutana na mwanamume kwa jina John Maina Ndegwa, aliyejitambulisha kama “wakili wa Kang’ethe”.

“Mwanamume aliyejitambulisha kama wakili wa Kang’ethe aliwasili kwenye kituo mwendo wa saa kumi jioni na kusema anataka kuzungumza na mteja wake,” ilisema taaarifa ya polisi.

“Maafisa walikubali ombi lake, wakamtoa mshukiwa ndani ya seli na kumwacha pekee yake na wakili wake katika chumba tofauti. Baada ya dakika chache, mshukiwa alifululiza nje.”

Katika kinachoweza tu kuelezewa kama sinema ya mchana, mshukiwa aliondoka kijasiri kutoka Kituo cha Polisi cha Muthaiga, kilichokuwa na maafisa wanne kwenye zamu, kabla ya kuabiri matatu na kuchana mbuga.

Kufikia sasa, wakili na maafisa wanne waliokuwa kwenye zamu wakati Kevin alitoweka korokoroni wamezuiliwa na polisi huku maswali yakizuka kuhusu ni vipi mshukiwa aliweza kuwakwepa kirahisi walinda usalama hao.

Maafisa hao ni pamoja na walinzi wawili wa kituo, Hassan Saman  na Ann Wanjiku, Mlinzi wa Seli, Elijah Kipkiror na Afisa wa Taarifa, James Maina.

Kang’ethe anashukiwa kumuua mpenzi wake raia wa Kenya aliyekuwa na umri wa miaka 31, na ambaye alikuwa mkazi wa eneo la Whitman, Massachusetts nchini Marekani mnamo Novemba 2023.

Mwili wa marehemu ulipatikana ndani ya gari katika Uwanja wa Ndege wa Logan ulioko Boston.

Kabla ya tukio hilo la kutatanisha, Kang’ethe alikuwa anasubiri kujua hatima yake kuhusu iwapo angesafirishwa hadi Marekani ambapo angefunguliwa mashtaka ya mauaji.

Mshukiwa alikamatwa jijini Nairobi ambapo makachero waliomba azuiliwe kwa muda wa siku 30 wakisubiri uamuzi.

  • Tags

You can share this post!

Nampenda mke wangu, tatizo ni kuwa ameniambia hana mpango...

Mume jasiri araruliwa na simba akiokoa mkewe

T L