Habari za Kitaifa

Getumbe kufikishwa kortini kwa kudaiwa ‘kuchafua hewa’

March 12th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA FRIDAH OKACHI

MWANAMUZIKI wa Injili William Getumbe anatarajiwa kufikishwa mahakamani Ijumaa baada ya kujipata matatani kwa kuimba wimbo ambao inadaiwa ulichafua hewa.

Mwanamuziki huyo ambaye alimulikwa na Bodi ya Uainishaji Filamu Nchini (KFCB) alikamatwa Jumatatu, lakini akaachiliwa kwa bondi ya polisi ya Sh10,000.

Alikuwa amenyakwa na maafisa wa kituo cha polisi cha Kapsoya kwa kukaidi maagizo ya KFCB.

Katika mahojiano na Taifa Leo, Bw Getumbe alisema alilipa bondi ya polisi Jumanne asubuhi ili kuwa huru.

“Niliambiwa kosa langu ni kuzalisha filamu bila leseni lakini ukiangalia nyimbo zangu, mimi sio mzalishaji wa filamu,” akadai Bw Getumbe.

Mwimbaji huyo wa wimbo uliozua utata wa ‘Yesu Ninyan***’ alielezea jinsi ambavyo alikamatwa usiku akiwa nyumbani kwake.

“Nilikuwa ninajiandaa kulala niliposikia ngo! ngo! ngo! kwa mlango. Nilipoenda kuufungua, polisi walinimyaka na kuniambia niandamane nao hadi kituo cha polisi,” akasimulia.

Mwanasaikolojia huyo amepiga madai ya kukaidi maagizo ya KFCB.

Alisema hakuona haja ya kufika mbele ya bodi hiyo baada ya nyimbo zake nane kufutwa kwenye chaneli ya YouTube.

“Katika maagizo waliotuma kwangu, hakuna sehemu waliotaja kwamba ninafaa kufika mbele ya bodi hiyo. Waliniagiza tu nifute muziki ambao walitaja haufai na kuniagiza kulipa Sh6 milioni,” akaeleza.

Mnamo Machi 6, 2024, baba huyo wa watoto wanne alielekea katika Mahakama ya Milimani, kupinga maagizo hayo pamoja na ngoma zake kufutwa.

“Wiki jana nilienda mahakamani nikiandamana na wakili wangu jijini Nairobi kutokana na maagizo waliyonipa. Jaji alitoa mwelekeo na kunipa barua lakini sasa kwa kunikamata, KFCB imeonyesha ukiukaji mkubwa,” akaongeza kulalama.

Alisema sasa baada ya kamatakamata iliyomnasa, sasa anasubiri kuona jinsi mambo yatakavyoenda Ijumaa.

“Nilivyoelekezwa, nitahitajika kufika mbele ya korti mnamo Ijumaa au Jumatatu,” akasema.

KFCB ilimkamata mwanamuziki huyo baada ya siku saba za makataa aliyowekewa kutamatika.

Katika taarifa iliyotumwa na bodi hiyo, ilisema kuwa mwambaji huyo alikiuka kifungu cha filamu na michezo jukwaani cha 22 kulingana na Katiba.

Bw Gitembe atafikishwa mbele ya makama na kushtakiwa kwa makosa matatu. Kosa la kwanza likiwa ni kuzalisha filamu bila leseni kinyume na sheria.

Kosa la pili ni kusambaza nyenzo za filamu na sauti kinyume cha sheria ambapo pia alimiliki na kusambaza filamu chafu hadharani bila kujali inadunisha maadili ya kijamiii. Kosa la tatu ni kuvalia suruali aina ya Diapers, hatua ambayo kulingana na sheria za KFCB ilikiuka maadili ya kuficha uchi wa binadamu ambaye tayari ni mtu mzima.