Habari za Kitaifa

Mwanasiasa ni kati ya watu 3 waliotiwa kizuizini kuhusu mauaji ya wakili Mbobu

Na  WAANDISHI WETU September 13th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MWANASIASA mmoja na watu wengine wawili wamekamatwa kuhusiana na mauaji ya wakili Kyalo Mbobu, huku polisi wakiendelea kuchunguza simu ya marehemu pamoja na ushahidi mwingine kutafuta vidokezo zaidi.

Watatu hao walikuwa miongoni mwa watu wa mwisho kuonekana na Bw Mbobu akiwa hai, walipokutana katika hoteli moja jijini Nairobi mnamo Jumanne iliyopita, saa chache tu kabla wakili huyo kuuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana.

Wote hao, ambao walikamatwa mwendo wa saa saba usiku kuamkia jana, ni majirani wa marehemu. Mmoja wao alikuwa na mazoea ya kufanya mazoezi ya kukimbia na Bw Mbobu kila asubuhi.Wakili anayemwakilisha mwanasiasa huyo alithibitisha kukamatwa kwa watu hao lakini akasisitiza kuwa kwa sasa ni “watu wa kutiliwa shaka” tu na bado hawajashtakiwa rasmi.

Mwanasiasa huyo alipelekwa hospitalini baada ya kudai anahisi vibaya akiwa chini ya ulinzi wa maafisa polisi.Bw Mbobu alishambuliwa na wanaume wawili kwenye pikipiki Jumatano jioni akielekea nyumbani kwake Karen kupitia barabara ya Magadi.

Mmoja wao alimpiga risasi mara nane. Siku ya Alhamisi, Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen alisema kuwa uchunguzi unawahusisha watu wengi wanaoshukiwa.“Tunaelezwa kuwa ni uchunguzi wa mauaji unaoendelea, lakini bado hatujapewa maelezo rasmi ya mashtaka.

Huu ni uchunguzi mpana na polisi bado hawajabainisha iwapo mteja wangu atahusishwa moja kwa moja,” alisema wakili huyo alipokuwa katika kituo cha polisi cha Kileleshwa, ambako mteja wake alikuwa amefungiwa.

Baada ya kukamatwa, watatu hao walihojiwa kwa saa kadhaa katika afisi za Kitengo cha Mauaji, Nairobi. Mwanasiasa huyo alizuiliwa Kileleshwa, huku mshukiwa mwingine akihamishiwa kituo cha polisi cha Capitol Hill. Haijabainika mshukiwa wa tatu anazuiliwa wapi.

“Tunaambiwa kuwa kuna watu wengi wanaochunguzwa. Kwa sasa mteja wangu anaonekana kama mtu wa kushukiwa tu. Tunangojea stakabadhi rasmi,” akaongeza wakili huyo.Bw Mbobu alishambuliwa na wanaume wawili waliokuwa kwenye pikipiki, Jumatano jioni, akiwa njiani kuelekea nyumbani kwake Karen kupitia barabara ya Magadi. Mmoja wao alimpiga risasi mara nane.

Chanzo cha polisi kilisema kuwa uchambuzi wa kielektroniki wa simu ya marehemu unaendelea, na katika awamu ya awali, uchunguzi huo uliwaelekeza kwa watu hao watatu waliokamatwa.Maafisa wa upelelezi pia wanawachunguza watu wengine wawili – mwanamke aliyekuwa akiwasiliana naye mara kwa mara kwa simu, na mwanaume aliyemzungumza kwa takriban dakika 10 siku aliyouawa.Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) bado haijatoa taarifa rasmi kuhusu hatua iliyofikiwa kwenye uchunguzi huo.

Hata hivyo, siku ya Jumatano, DCI ilitoa wito kwa umma kutoa taarifa yoyote yenye kusaidia katika kuchunguza tukio hilo

.“DCI imejitolea kuhakikisha wahusika wa tukio hili la kikatili wanakabiliwa na mkono wa sheria. Timu yetu ya wachunguzi inafanya kazi kwa bidii, kwa kutumia rasilmali na ujuzi wote uliopo,” alisema Mkuu wa DCI Mohamed Amin katika taarifa.Siku ya Alhamisi, Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen alisema kuwa uchunguzi unawahusisha watu wengi wanaoshukiwa.