Mwandani wa Gachagua ajiondoa kabla ya kutimuliwa
SENETA wa Laikipia John Kinyua amejiuzulu wadhifa wake kama mwanachama wa Tume ya Huduma za Bunge (PSC).
Bw Kinyua amechukua hatua hiyo kufuatia fununu kwamba baadhi ya wabunge na maseneta waliopinga hoja ya kumtimua aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua watapokonywa nafasi wanazoshikilia katika kamati zenye ushawishi bungeni.
Seneta huyo anayehudumu muhula wa pili, ni mwandani wa Bw Gachagua na ni miongoni mwa wale waliopinga mashtaka yote yaliyokuwa kwenye hoja hiyo iliyodhaminiwa na Mbunge wa Kibwezi Mwengi Mutuse.
Kiongozi wa wengine katika Seneti Aaron Cheruiyot ndiye alifichua habari kuhusu kujiuzulu kwa Seneta Kinyua wakati wa kikao cha Jumanne, Novemba 19.
Hata hivyo, Bw Cheruiyot ambaye ni Seneta wa Kericho, hakuelezea sababu zilizochangia kujiuzulu kwa Bw Kinyua.
Baada ya kutoa tangazo hilo, Kiongozi huyo wa Wengi alisoma taarifa akiijulisha Seneti kwamba Seneta wa Nyeri Wahome Wamatinga ndiye atajaza nafasi ya Kinyua katika PSC.
“Imeamuliwa kwamba Seneta wa Nyeri Wahome Wamatinga ateuliwe kuwa kamishna kujaza nafasi ya Seneta wa Laikipia John Kinyua ambaye alijiuzulu,” ikisema taarifa hiyo ilisomwa na Bw Cheruiyot.
PSC inaongozwa na Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula huku ikiwa na wanachama wengine 10.
Naibu wake ni Seneta Maalum Joyce Korir. Wanachama wengine ni pamoja na wabunge; Mishi Mboko (Likoni), Patrick Makau (Mavoko), Faith Gitau (Mbunge Mwakilishi Nyandarua) na Mohamed Ali (Nyali).
Wengine ni; Seneta Okong’o Omogeni, Seneta wa zamani wa Machakos Johnson Muthama, aliyekuwa Mbunge Mwakilishi wa Kakamega Rachel Meson na Karani wa Seneti John Nyengenye, ambaye ni Katibu wa PSC.
Tume hiyo huajiri wafanyakazi wa asasi ya bunge, hutoa huduma na vifaa vya kuwezesha asasi hiyo kuendesha majukumu yake ipasavyo.