Habari za Kitaifa

Mwandani wa Gachagua kuhojiwa na DCI baada ya kudai serikali inaua Gen Z

Na CHARLES WASONGA July 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MBUNGE wa Naivasha, Jayne Kihara, ameagizwa kufika mbele ya wapelelezi katika Makao Makuu ya Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI), Jumba la Mazingira, Barabara ya Kiambu, Nairobi, leo kuhusiana na madai kuwa alichochea chuki.

Kulingana na agizo hilo, Mbunge alitoa kauli ambazo zinaweza kuwafanya raia kuwachukia maafisa wenye mamlaka serikalini.

“Kitengo cha uchunguzi katika DCI kilichoko katika makao makuu kinachunguza madai ya kosa la kuhujumu mamlaka ya afisa wa umma kinyume na sehemu 132 ya Sheria ya Uhalifu, Sura ya 63 ya Sheria za Kenya baada ya malalamishi kuhusu usambazaji wa kauli za uchochezi kuwasilishwa,” ikasema hati ya agizo hilo iliyotiwa saini na Naibu Mkurugenzi wa Kitengo cha Uchunguzi, George Lenny Kisaka.

“Ninayo sababu ya kuamini kuwa wewe, Jayne Njeri Kihara, Mbunge wa Naivasha, unahusika na kosa hilo au unayo maelezo yanayoweza kunisaidia katika uchunguzi wangu,” akaongeza Bw Kisaka, ambaye pia ni Msaidizi wa Inspekta Jenerali wa Polisi.

Kwa hivyo, afisa huyo anamtaka Mbunge huyo kufika mbele yake afisini mwake katika makao makuu ya DCI, leo, Jumatatu Julai 14, 2024, saa nne na nusu asubuhi, kudadisiwa kuhusiana na suala hilo la madai ya kutoa matamshi ya chuki.

“Zingatia kwamba ukifeli kufika kulingana na agizo hili, utakuwa umetenda kosa ambalo adhabu yake ni kifungo gerezani chini ya sheria husika,” Bw Kisaka akamwonya Bi Kihara.

Lakini Mbunge huyo alikuwa mwepesi kudai kuwa DCI inamwandama kutokana na kauli kali ambazo amekuwa akitoa akiilaumu serikali kuhusiana na mwenendo wa polisi kuwaua raia kiholela nyakati za maandamano katika siku za hivi karibuni.

“Nadhani ni kuhusiana na hutoba yangu wakati wa mazishi ya Boniface Kariuki katika Kaunti ya Murang’a mnamo Ijumaa ambapo nilisema wazi kwamba serikali ndiyo ya kulaumiwa kwa kifo cha kijana huyo,” akasema Bi Kihara, ambaye ni mwandani wa aliyekuwa Naibu Rais, Rigathi Gachagua.

Marehemu Kariuki, ambaye alikuwa muuzaji wa barakoa, alipigwa risasi na polisi katikati mwa jiji la Nairobi mnamo Juni 17, wakati wa maandamano ya kulaani mauaji ya mwanablogu Albert Ojwang’.

Alikufa mnamo Juni 30, siku 13 baada ya kulazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) na akazikwa mnamo Ijumaa ya Julai 11, 2025 nyumbani kwao katika eneobunge la Kangema, Kaunti ya Murang’a.