Mwaniaji wa Farouk, Kindiki mchujo wa UDA Baringo aangushwa na ‘mgeni’ Chemitei
KWA mara ya kwanza katika historia ya siasa za Baringo, mwaniaji kutoka jamii ndogo iliyobaguliwa ya Endorois amepenya na kuwashinda wanaotoka jamii kubwa ya Tugen.
Vincent Kiprono Chemitei, 31, ambaye alishinda mchujo wa UDA wikendi sasa huenda akawa kiongozi wa kwanza wa jamii hiyo kuwa seneta iwapo atashinda uchaguzi mdogo wa Novemba 27 mwaka huu.
Lilikuwa tukio la kihistoria kwa Bw Chemitei kutoka jamii ndogo kuibuka mshindi wa mchujo huo, akiwabwaga wapinzani wake wengine wanane kutoka jamii ya Tugen.
Bw Chemitei sasa anaonekana yupo guu moja kuingia katika Bunge la Seneti baada ya kuangusha wawaniaji wengine ambao walioonekana kuwa na uwezo mkubwa wa fedha na uungwaji mkono wa vigogo.
Ushindi wake unaonekana kama pia wa Pokot, Ilchamus, Turkana, Agikuyu na Wanubi ambao wamekuwa wakibaguliwa na kulemewa katika siasa za Baringo kutokana na idadi yao ndogo.
Tangu kuanzishwa kwa mfumo wa ugatuzi, jamii ya Tugen imepata ushindi kwenye nyadhifa zote za uongozi katika kaunti hiyo.
Kwenye uchaguzi wa 2022, kiti cha ugavana kilitwaliwa na Benjamin Cheboi, Mbunge Mwakilishi wa Kike akawa Florence Jematia na kiti cha seneti ambacho sasa kinawaniwa kikamwendea marehemu William Cheptumo.
Kwenye mchujo wa UDA uliokamilika, Bw Chemitei alizoa kura 48,791 dhidi ya Wycliffe Kipsang Tobole ambaye alipata kura 30,897 kisha Daniel Kiptoo maarufu kama DK akapata kura 23,613.
Wengine walioshiriki mchujo huo ni Silas Tochim (769), Evans Mundulel (735), Joseph Cherutoi (172), Isaiah Kirukmet (141), Lineus Kamket (118) na Reuben Chepsongol (82).
Kando na Bw Chemitei, wawaniaji wengine wote walikuwa kutoka jamii ya Tugen. Kwa mujibu wa mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Kevin Keitany kutoka Kaunti Ndogo ya Mogotio, ushindi wa Bw Chemitei unaamanisha kuwa jamii ndogo zikiungana zitakuwa na usemi mkubwa katika siasa za kaunti hiyo.
“DK alikuwa akipigiwa upatu na alisemekana alitumia mamilioni ya pesa kwenye kampeni lakini akabwagwa. Hii pia inaonyesha kuwa raia wana usemi katika siasa za Baringo kwa sababu Bw Kiptoo alikuwa akiungwa mkono na baadhi ya vigogo wa UDA,” akasema Bw Keitany.
“Uwezo wake wa kuongea lugha za jamii za Pokot, Tugen, Arror na Kikuyu kulifanya achangamkiwe na wapiga kura kutoka jamii zote,” akaongeza.
Bw Chemitei aliwashukuru wapiga kura kwa kutokuwa na miegemeo ya kijamii waliposhiriki mchujo huo wa chama cha UDA.
“Ushindi huu ni wenu na ninatoa ahadi kuwa nikishinda kiti hiki cha useneta nitatumikia jamii zote ndani ya Baringo kwa usawa,” akasema.
Pia alishukuru UDA kwa kuandaa mchujo huru huku akitoa wito kwa viongozi wote wa ngazi ya juu kumuunga mkono apate kiti hicho.