Mwili wa mwalimu mkuu aliyetoweka akiendea KCSE wapatikana mtoni
Polisi katika kaunti ya Kakamega wameanzisha uchunguzi kuhusu kifo cha mkuu wa shule ambaye mwili wake ulipatikana katika Mto Kipkaren, siku kadhaa baada ya kupotea.
Mwili wa Simon Isiaho Shange, mkuu wa Shule ya Sekondari ya Munyuki, ambaye alipotea Jumatatu iliyopita, Novemba 3, ulipatikana Jumamosi, Novemba 8 ukiwa umetupwa mtoni.
Bw Isiaho alipotea asubuhi ya Jumatatu alipokuwa akienda kuchukua karatasi za mtihani kutoka ofisi ya Naibu Kamishna wa kaunti ndogo ya Lugari.
Kamanda wa polisi wa Lugari, Robert Kurgat, alisema kugunduliwa kwa mwili wa mwalimu huyo kumemaliza msako uliofanywa na familia yake, walimu, wakazi wa eneo hilo, na mamlaka.
Bw Kurgat alisema wanachukulia tukio hili kama mauaji hadi uchunguzi utakapothibitisha vinginevyo.
‘Hata hivyo, tunaomba utulivu kwa sababu maafisa wetu kutoka kwa Idara ya Uchunguzi ya Makosa ya Jinai (DCI) wameanzisha uchunguzi wa kina ili kugundua wahusika,’ alisema Bw Kurgat.
Maafisa kutoka DCI walikusanya sampuli katika eneo ambapo mwili wake ulipatikana na kuhoji wakazi wa eneo hilo.
Uchunguzi wa awali ulibaini uwezekano wa Mkuu wa Shule huyo kuteswa kabla ya kuuawa.
Kupotea kwa mwalimu huyo kulisababisha maandamano makubwa katika Kakamega huku viongozi wa KUPPET wakitishia kuvuruga mtihani wa KCSE unaondelea.
Naibu Gavana wa Kakamega Ayub Savula aliwaomba polisi kufanya uchunguzi wa kina na kuwakamata washukiwa wote.