• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 9:50 AM
Naibu Inspekta Jenerali wa polisi asimulia korti jinsi alivyotiliwa ‘mchele’ na kupoteza Sh1.5m

Naibu Inspekta Jenerali wa polisi asimulia korti jinsi alivyotiliwa ‘mchele’ na kupoteza Sh1.5m

NA RICHARD MUNGUTI

ALIYEKUWA Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi ametoa ushahidi wake mbele ya mahakama ya Nairobi akieleza jinsi ambavyo aliwekewa ‘mchele’ kwa kinywaji katika kilabu kimoja Juja kabla ya kuibiwa Sh1.5 milioni.

Bw Paul Maingo aliambia hakimu wa mahakama ya Milimani Lucas Onyina, kwamba alitiliwa mchele na mwanamke aliyejitambulisha kama Jane ambaye alisema alikuwa akifanya kazi nchini Marekani na kwamba wakati huo alikuwa katika likizo nchini.

Alisema kwamba rafiki yake alimtaka kumpeleka nyumbani kwake eneo la Ruiru kwa gari lake rasmi na alipotoka huko, akaingia kwa kilabu cha DJ Club kilichoko Juja akaitisha kinywaji.

Dakika chache baadaye wanawake wawili na mwanamume waliingia na kuketi kwa meza iliyokuwa karibu na ya Bw Maingo.

“Mwanamke mmoja wao alinikujia na kuomba ajiunge name kwa meza name nikakubali. Ninachokumbuka ni kwamba aliniambia alikuwa akifanya kazi nchini Marekani,” akasema Bw Maingo.

Alipoteza fahamu.

Aliambia mahakama kwamba kesho yake alijipata kwa gari lake hatua kama kilomita moja hivi kutoka kwa kilabu hicho na “sikujihisi vizuri kwa sababu nilikuwa nimetapika ndani ya gari na nilihisi kizunguzungu”.

“Nilikuwa upande mkono tofauti na usukani na gari lilikuwa likinguruma,” akaiambia mahakama.

Aligundua kwamba alikuwa amepoteza simu mbili, moja ya Samsung S 22 na nyingine ya Samsung S 9.

Pia alikuwa amepoteza saa ya mkononi.

Simu na saa vyote vilikuwa vya thamani ya Sh305,000.

Aidha, alikuwa pia amepoteza kadi mbili za Absa za kupata huduma kwa mashine za ATM, kitambulisho cha kitaifa na kibeti kilichokuwa na ShSh15,000 na stakabadhi za kibinafsi.

Aliendesha gari hadi nyumbani na dereva wake–koplo Mwangangi—alipowasili, alitumia simu yake kupigia benki ya Absa.

Baadaye benki ilimfahamisha Sh1,154,084 zilikuwa zimetolewa kwa akaunti yake.

Alitibiwa kwa hospitali ya Belleview South ambapo ripoti ilitiwa saini na Dkt A Valerie.

Aliripoti kwa kituo cha polisi cha Ruiru na kile cha KICC huku akimalizia kwa kuwapa maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) katika makao makuu yaliyoko Kiambu Road.

Washukiwa wanne walikamatwa.

Walioshtakiwa ni Evelyn Wambui Mutura almaarufu Jane, Janet Wanjiru Ngugi, David Wanjogo Kariuki, na Ibrahim Mwangi Kiria.

Wanadaiwa kutekeleza makossa hayo mnamo Machi 20 na Machi 21, 2023, katika DC Club, Kimbo, Juja.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Khalwale amtaka Toto afute ‘uongo’ mitandaoni...

Mahakama yazuia LSK kufanya uchaguzi wa mwakilishi katika...

T L