Habari za Kitaifa

Nairobi, Mombasa na Kisumu kupata mvua siku tano

Na BENSON MATHEKA January 1st, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MAENEO kadhaa yatapata mvua za hapa na pale huku maeneo mengi ya nchi yakiendelea kukumbwa na hali ya jua na ukame kwa muda wa siku tano hadi Januari 5, idara ya Hali ya Hewa ya Kenya imetangaza January 1 2025.

Katika utabiri wa kila wiki idara ilisema kuwa Kaunti za Nairobi, Kisumu na Mombasa zitapata mvua ya mara kwa mara.

Wakenya wanaoishi katika kaunti za Nyandarua, Laikipia, Nyeri, Kirinyaga, Murang’a, Kiambu, Meru, Embu na Tharaka pia watapata mvua za hapa na pale.

Kwa mujibu wa idara ya hali ya hewa, mvua katika maeneo hayo inatabiriwa kunyesha mchana, huku maeneo machache yakipata mvua asubuhi.

Nyanda za Juu Magharibi mwa Bonde la Ufa, Bonde la Ziwa Victoria, na Bonde la Ufa la Kati zitapokea mvua ikiandamana na radi katika maeneo machache.

“Mvua ya mara kwa mara inatarajiwa katika eneo la Pwani na katika baadhi ya Nyanda za Juu Magharibi na Mashariki za Bonde la Ufa, Bonde la Ziwa Victoria, Bonde la Ufa Kusini, na nyanda za chini za Kusini-mashariki,” idara ilisema katika toleo lake la kila wiki.

Vile vile, Wakenya wanaoishi katika kaunti za Siaya, Kisumu, Homabay, Migori, Kisii, Nyamira, Trans Nzoia, Baringo, Uasin Gishu, Elgeyo-Marakwet, na Nandi walishauriwa wajitayarishe kwa mvua mara kwa mara katika muda wa siku tano zijazo.

Zaidi ya hayo, wakazi wa Kaunti za Kilifi, Lamu na Kwale, pamoja na sehemu za pwani za Kaunti ya Tana River, pia walishauriwa wajitayarishe kwa hali kama hiyo na vipindi vya jua asubuhi.

Wakati huo huo, idara ya utabiri wa hali ya anga katika ushauri wake pia ilionya kuhusu joto kali, haswa katika kaunti za Kaunti za Kaskazini Mashariki.

Hata hivyo, Kaunti za Kaskazini-magharibi zikiwemo Turkana na Samburu, hazitapata mvua yoyote.