Nairobi yaongoza kitaifa kwa maambukizi ya HIV kwa mara ya kwanza – Ripoti
KWA mara ya kwanza baada ya miaka mingi, Kaunti ya Nairobi imeipiku Homa Bay kwa kuongoza, kitaifa, katika idadi ya maambukizi mapya ya virusi vya HIV na ugonjwa wa Ukimwi.
Kwa mujibu wa data kutoka kwa Baraza la Kitaifa la Kudhibiti Magonjwa ya Kuambikizana (NSDCC), Kaunti ya Nairobi iliandikisha jumla ya maambukizi mapya 3,045 ya ugonjwa huo katika mwaka jana.
Kaunti ya Migori ilishikilia nambari mbili kwa kuandikisha jumla ya maambukizi 1,572 ikifuatwa na Kisumu iliyokuwa na jumla ya watu 1,341 walioambukiwa Ukimwi katika mwaka huo.
Kwa miaka mingi, kaunti za Homa Bay, Migori, Kisumu na Siaya, mtawalia, zimekuwa zikiongoza kwa maambukizi mapya ya Ukimwi.
Kulingana na NSDCC, kiwango cha maambukizi mapya ya Ukimwi kitaifa, kilipanda kwa asilimia 19, kutoka watu 16,752 mnamo 2023 hadi watu 19,991 mwaka jana.
Aidha, jumla ya kaunti 10 za Nairobi, Migori, Kisumu, Homa Bay, Busia, Siaya, Kakamega, Nakuru, Mombasa na Bungoma, zilichangia asilimia 60 ya maambukizi mapya katika mwaka huo wa 2024.
“Kwa wastani, kiwango cha maambukizi ya Ukimwi kitaifa kilikuwa ni asilimia 3.0 huku jinsia ya kike ikiandikisha maambukizi ya juu ya asilimia 4.0 ikilinganishwa na asilimia 2.0 miongoni wa watu wa jinsia ya kiume katika mwaka wa 2024,” ikaeleza ripoti hiyo kwa jina “Kenya HIV Estimates” iliyotolewa na NSDCC jana, siku moja kabla ya Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani leo hii.
Aidha, ripoti hiyo ya uchunguzi inaonyesha kuwa idadi ya vifo kutokana na ugonjwa huo iliongezeka kwa kiwango cha 0.05 mnamo 2024 kwani ni vifo 21,007 viliandikishwa.
Hii ilikuwa ongezeko kutoka jumla ya vifo 18,473 vilivyoandikisha katika mwaka uliotangulia wa 2023.
“Jumla ya vifo 21,000 vinavyotokana na Ukimwi vilivyoandikishwa mnamo 2024, inatukumbusha kuhusu haja ya juhudi kuongezwa kuwahamasisha watu kupimwa mapema, kuzingatia taratibu za matibabu na utunzaji watu wanaoishi na ukimwi,” akasema Katibu wa Afya ya Matibabu Ouma Oluga.
Lakini kuna mwanga wa matumaini kwani data hiyo ya NSDCC inaonyesha kuwa idadsi Kenya iliandikisha punguza.
Hadi mwaka wa 2024, jumla ya Wakenya 1,326, 336 walikuwa wakiishi na virusi vya HIV, 62,798 miongoni mwao wakiwa watoto.
Data ya NSDCC pia inaonyesha kuwa idadi ya maambukizi mapya inasalia juu miongoni mwa vijana wenye umri wa kati ya miaka 15 na 34.
Kwa upande mwingine kulingana na ripoti hiyo, idadi ya maambukizi mapya ilipungua kwa kima cha asilimia 75 katika kaunti za Elgeyo-Marakwet, Wajir, Mandera, Kisii, Machakos, Kericho, Uasin Gishu, Nakuru, Bomet, Baringo, Trans-Nzoia na Laikipia.