• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 8:55 PM
Nakhumicha ataka hospitali zikubali NHIF akisema madeni yote yatalipwa

Nakhumicha ataka hospitali zikubali NHIF akisema madeni yote yatalipwa

NA WINNIE ONYANDO

WAZIRI wa Afya, Susan Nakhumicha, Jumatano alitoa wito kwa vituo vya Afya nchini kuwahudumia wagonjwa wanaotumia Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Afya (NHIF) akisisitiza kwamba serikali italipa madeni ya hazina hiyo.

Waziri huyo alisema hayo jana alipofika mbele ya Kikao cha bunge lote kujibu maswali kuhusu mgomo wa madaktari miongoni mwa masuala mengine.

Alibainisha kuwa deni ambalo vituo mbalimbali vya afya linadai NHIF litalipwa pindi tu Hazina ya Kitaifa itakapotoa fedha hizo.

“Nataka kuvihakikishia vituo vya afya nchini kwamba tutalipa madeni yote. Hivyo hakuna haja ya kuwanyima huduma wagonjwa wanaotumia kadi ya NHIF. Kwa sasa tunasubiri fedha kutoka kwa Hazina ya Kitaifa,” akasema.

Nakhumicha alifichua kuwa Hazina ya Kitaifa inatarajiwa kutoa Sh8.5 bilioni hivi karibuni, ambazo zitatumika kulipa madeni ambayo vituo mbalimbali vya afya vinadai.

Haya yanajiri huku kukiwa na ripoti kwamba wagonjwa walio na kadi za NHIF wananyimwa huduma za kimatibabu kutokana na madai ya malimbikizo ya madeni ya serikali ya jumla ya takriban Sh6 bilioni.

Shirikisho la Afya nchini mwezi jana lilisema kwamba iwapo serikali haitalipa madeni basi wagonjwa wanaotumia kadi ya NHIF watalazimika kugharamia matibabu yao.

Shirikisho hilo lilisema kwamba watakaofika hospitalini au kwenye vituo vya afya wakiwa na kadi hiyo watahitajika kulipa pesa taslimu ili kuhudumiwa.

Haya yanajiri huku serikali ikijiandaa kutekeleza Sheria ya Hazina ya Afya ya Kijamii (SHIF).

Hata hivyo, Waziri Nakhumicha alishikilia kwamba Wakenya wataendelea kulipa NHIF hadi SHIF itakapoanza kutekelezwa.

Wakati uo huo, waziri huyo alisema kuwa hawezi kutoa muda mahususi au tarehe ambapo mgomo wa madaktari nchini utatatuliwa.

“Ndiyo, tunafahamu mgogoro unaoendelea nchini. Siwezi kutoa tarehe au wakati mahususi ambapo mgomo utaisha. Tunajaribu tuwezavyo na sasa hivi, tuko kwenye mchakato wa mazungumzo,” CS Nakhumicha aliambia Seneti.

Mgomo huo ulianzishwa na madaktari mnamo Machi 15, 2024.

  • Tags

You can share this post!

Wafanyabiashara Uganda wagoma kupinga mfumo mpya...

Wizara yatoa onyo la mafuriko mabwawa ya Masinga, Kindaruma...

T L