• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Natembeya analenga kiti cha urais 2032?

Natembeya analenga kiti cha urais 2032?

NA FRANCIS MUREITHI

TANGU afisa wa zamani wa utawala George Natembeya aliposhinda ugavana wa Trans Nzoia ameendelea kuibua maswali mengi kwa kutikisa wananasiasa wakuu wa Magharibi mwa Kenya Musalia Mudavadi na Moses Wetang’ula.

Bw Natembeya, ambaye hadi miezi michache kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022 alikuwa Kamishna wa Bonde la Ufa, anaonekana kuibuka kama mwanasiasa anayetaka kutwaa taji la msemaji wa jamii ya Mulembe.

Aidha, jambo hili geni katika ulingo wa siasa, amejitokeza kama mwanasiasa anayepania kutimiza ndoto ya miaka mingi kufanikisha umoja wa jamii ya Waluhya.

Sasa swali lililoko vinywani mwa wengi ni hili; je, atafaulu kutimia ndoto hii ambayo imelemea Mudavadi na Wetang’ula na hata Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi Nchini (Cotu) Francis Atwoli?

Huku akionekana kujibu swali hili, na mengine ambayo yamezua kizungumkuti katika siasa za Magharibi mwa Kenya, Bw Natembaya anaonekana kutumia tajriba yake ya muda mrefu katika utawala wa mkoa kujijengea himaya ya siasa.

Kwa mfano, amejijengea sifa kama kamishna wa kipekee wa Bonde la Ufa aliyefaulu kuwafurusha walowezi kutoka Msitu wa Mau na kukabiliana vikali na majangili na wafuasi wa kundi haramu la Mungiki kwa kutumia mbinu za Makomando.

Inaaminika kuwa Bw Natembeya anapania kutumia mbinu kama hizo kuendeleza mikakati ya kumwezesha kutwaa taji la msemaji wa jamii ya Waluhya.

Ilivyokuwa alipohudumu katika utawala wa mkoa, Gavana huyo wa chama cha DAP-Kenya, anaonekana kama mchapakazi na hutia bidii katika kile anachotaka kufikia.

Na sasa ameanzisha kampeni ya kujinadi sio tu kama kiongozi wa jamii ya Waluhya bali kama mtetezi wa watu maskini katika jamii hiyo.

Katika hotuba zake za kisiasa na kutangamana kwake na watu, akishiriki nao vyakula na vinywaji, Bw Natembeya anajitokeza kama “mtu wa watu”.

Huku uchaguzi mkuu wa 2027 ukielekea ukweli kuhusu nyota na sifa za kisiasa Natembeya utabainika.

Kwa mfano, Gavana huyo ameahidi kutekeleza mageuzi katika ulingo wa siasa katika eneo la Mulembe inapojiandaa kudhamini mmoja wao kuwania urais 2032.

Bw Natembeya amesema kuwa huo ndio wakati mwafaka kwake kuingia Ikulu.

Ameahidi vita kali dhidi ya vyama vikuu eneo la Magharibi ambavyo ni; Ford Kenya na ANC.

Kwa mfano, anasema Ford Kenya inayoongozwa na Bw Wetang’ula imefeli kwa kushindwa kutetea maslahi ya jamii ya Waluhya kwani mamilioni ya watu wake wanazongwa na umaskini, ukosefu wa ajira na kupanda kwa gharama ya maisha.

Hata hivyo, wadadisi wanasema Bw Natembeya, 53, ana kibarua kikubwa kufikia ndoto ya kuunganisha jamii ya Waluhya, kuwa msemaji wao na hatimaye kuwa wa kwanza kutoka jamii hiyo kufaulu kuingia Ikulu.

Sawa na Rais William Ruto ambaye akiwa katika ngome yake ya Bonde la Ufa hutumia lugha yake ya Kikalenjin kusisitiza jambo, gavana huyu pia ameiga mfano huo na hugeukia lugha yake ya Kibukusu kusisitiza jambo.

Tulipomuuliza ikiwa atawania urais 2032, Bw Natembeya hakukana wala kukubali lakini alisema kuwa atahakikisha kuwa jamii ya Mulembe inadhamini mgombeaji.

“Sio lazima iwe ni mimi lakini nitakuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa jamii yetu iko katika meza ya ugavi wa mapato ya taifa hili,” akasema.

Ameanzisha vuguvugu kwa jina TAWE yenye alama ya X ya mikono ya kupambana na umaskini, njaa, ukabila na changamoto zote katika Kaunti ya Trans Nzoia na eneo pana la Magharibi mwa Kenya.

 

  • Tags

You can share this post!

Afueni kwa Wakenya bei ya mafuta ikishuka zaidi

Askari rungu wataka watengewe saa za kunywa pombe mchana  

T L