Natembeya sasa ataka Ichungwa aombe msamaha au amshtaki
MATAMSHI ya Mbunge wa Kikuyu Kimani Ichung’wa wakati wa mazishi ya mamake Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetangula yamemtia matatani.
Hii ni baada ya Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya kumtumia barua ya kutaka aombe msamaha ndani ya siku tatu au amshtaki kwa kile anachotaja kama matamshi ya uongo, yenye nia mbaya kwa lengo la kumharibia jina.
Kupitia kampuni ya mawakili ya Oringe Waswa and Opany, Gavana huyo alisema kuwa Bw Ichung’wa, ambaye ni Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa, ana siku tatu za kuomba radhi kupitia magazeti matatu ya kitaifa au amshtaki.
“Tunaandika barua hii kudai, jambo ambalo tunafanya, kukutaka kuomba radhi, katika toleo lijalo la magazeti ya Nation, Standard na Star kwa maneno tutakayoidhinisha katika jitihada za kupunguza uharibifu mkubwa uliotokea kwa mteja wetu,” inasema sehemu ya barua ya mawakili wa Bw Natembeya.
Gavana huyo anataka taarifa itakayochapishwa ya kuomba msamaha ifanywe kwa njia ya wazi sawa na matamshi yaliyosababisha malalamishi hayo.
“Mteja wetu anataka, ambalo kupitia barua hii tunafanya, kwamba ufanye hivi ndani ya siku tatu la sivyo utafunguliwa mashtaka.”
Wakati wa mazishi Ijumaa katika eneo bunge la Kabuchai kaunti ya Bungoma ambayo yalihudhuriwa na viongozi kadha akiwemo Rais William Ruto, mbunge huyo alidai kuwa Gavana Natembeya alikuwa miongoni mwa waliohusika na utekaji nyara wa Wakenya wakati wa utawala uliopita, aliohudumu kama Kamishna wa eneo la Bonde la Ufa.
“Maneno uliyotamka mbele ya umati mkubwa ulioelekeza kwa mteja wetu yalimaanisha na kueleweka kuwa mteja wetu ni muuaji, amekosa maadili, mfanyikazi wa umma asiyezingatia taaluma ambaye alikuwa akisimamia mauaji ya Wakenya na kuwatupa katika Mto Yala. Maneno hayo yalimaanisha kuwa mteja wetu ni mhusika mkuu wa mauaji ya Wakenya wasio na hatia wakati wa utawala uliopita,” barua inasema.
Suala la kutekwa nyara lilitawala ibada ya mazishi ya mama ya Wetangula baada ya Gavana Natembeya kumuomba Rais kukomesha tishio hilo, akisema kuwa familia za vijana waliotoweka zinaishi kwa hofu.
IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA