Habari za Kitaifa

NCCK ilivyoandaa kikao kuelimisha wanaume kuhusu dhuluma za kijinsia

Na NA KNA November 30th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

BARAZA la Makanisa Nchini (NCCK), limekuwa na kongamano linalolenga wanaume katika Kaunti ya Embu ili kushughulikia visa vinavyoongezeka vya dhuluma za kijinsia.

Kongamano hilo la siku tatu lililoanza Alhamisi, linanuia kuangazia visa vya wanaume walioambukizwa virusi vya Ukimwi ambavyo NCCK ilisema bila shaka vinaongezeka katika kaunti hiyo.

Wadau waliteta kuwa visa vya wanaume kudhulumiwa havipewi kipaumbele ikilinganishwa na vya wanawake huku jamii ikiwa na haraka kushutumu hadharani wanaume wanaohusika.

Mwenyekiti wa NCCK Kaunti ya Embu, Askofu Stephen Njogu, alisema wanaume wamekuwa wakiteseka kimya kwa muda mrefu na kwa sababu kadhaa ikiwa ni pamoja na aibu, kejeli na hofu ya kuonekana kuwa dhaifu.

Aliwahimiza wanaume wasihofie kuripoti dhuluma wanazofanyiwa na wake zao ili wapate suluhu.Kiongozi huyo wa kidini alisema enzi za wanaume kuteseka kimya kimya kutokana na mila potofu za kitamaduni kuwa wanaume hawawezi kudhulumiwa zimefika mwisho.

Alisema pia wataandaa mpango wa kuwafikia wanaume kwa nia ya kuweka mifumo imara ya mawasiliano katika kutoa taarifa na kupunguza maambukizi ya Ukimwi.

Mwenyekiti wa Chama cha Kitaifa cha Biashara na Viwanda ya Kenya (KNCCI) tawi la Embu Mugo Mate alisema dhuluma za jinsia haiachi tu madhara ya kudumu kwa waathiriwa kimwili, kiakili na kijamii bali pia kiuchumi.

Alisema ugonjwa wa Ukimwi pia huchangia kushuka kwa uzalishaji na pato la kiuchumi kwa waathiriwa na kuacha wanaowategemea katika hatari.

Mratibu wa shirika lisilo la kiserikali la Uraia Trust Sospeter Gitonga alitaka uchunguzi ufanywe ili kubaini kuenea kwa ugonjwa wa Ukimwi miongoni mwa wanaume katika kaunti hiyo.