Habari za Kitaifa

Ngirici naye amruka Ruto, amlaumu kuhusu miradi Kirinyaga

Na GEORGE MUNENE March 24th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MWENYEKITI wa Kampuni ya Mbegu Nchini Wangui Ngirici ameelekezea lawama utawala wa Kenya Kwanza akidai umetenga Kaunti ya Kirinyaga.

Bi Ngirici ambaye ni mwandani wa Rais William Ruto, wikendi alilalamika kuwa miradi mingi ya maendeleo iliyoanzishwa na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta, imekwama na hakuna dalili zozote za kuikamilisha.
“Hatubembelezi kwa sababu ni haki yetu kupata maendeleo kwa sababu tulichagua serikali hii,” akasema Bi Ngirici.
Akizungumza kwenye eneobunge la Mwea, mwakilishi huyo wa zamani wa kike wa Kirinyaga alilalamika kuwa wenyeji walikuwa wakiteseka kwa sababu miradi ambayo inastahili kuwanufaisha imekwama.
Alizua kumbukumbu za kampeni mnamo 2022 ambapo Rais Ruto aliahidi kufufua miradi yote iliyokwama ikiwemo barabara lakini hakuna chochote ambacho kimefanyika.
“Dawa ya deni ni kulipa na serikali hii lazima itimize ahadi zake kwa raia wa Kirinyaga,” akaongeza.
Wakati huo huo, Bi Ngirici alisema kwamba wakazi hawajachangamkia mfumo wa ufadhili wa elimu katika vyuo vikuu pamoja na Bima ya Afya ya Kijamii (SHA) akisema serikali inastahili kuziondoa.
“SHA na mfumo wa ufadhili wa elimu ya juu ni mbaya na serikali inastahili kutendea raia haki kwa kuziondoa,” akaongeza.
Bi Ngirici alitangaza kuwa atagombea kiti cha ugavana 2027 baada ya kupoteza 2022 kwa Anne Waiguru. Aliwania kama mgombeaji huru huku Bi Waiguru akitetea wadhifa wake kupitia chama tawala cha UDA.
Bi Ngirici aliwasilisha kesi kwenye Mahakama Kuu ya Kerugoya lakini akaondoa kesi hiyo baada ya kuteuliwa mwenyekiti wa kampuni ya mbegu.
Kwa wapinzani wake wa kisiasa, kiongozi huyo aliwataka wakome kupiga siasa kanisani na pia wakome kumtusi.
“Wanamimina matusi wala hawana heshima kwa maeneo ya kuabudu. Hata wanawapokonya wahubiri vipaza sauti,” akasema.
Mumewe Andrew Ngirici alisema kuwa sasa anaandamwa na maafisa wa Idara ya Upelelezi Nchini (DCI) kwa kukosoa serikali.
“Sitatishwa na nitaendelea kusema ukweli,” akasema Bw Andrew.

Imetafsiriwa na Cecil Odongo