• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
NHIF imeoza kwa ufisadi – Nakhumicha

NHIF imeoza kwa ufisadi – Nakhumicha

NA LUCY MKANYIKA

WAZIRI wa Afya Susan Nakhumicha amesema kuwa ufisadi katika bima ya afya (NHIF), ambayo itabadilishwa na Bima ya Kijamii ya Afya (SHIF), umesababisha Wakenya wengi kukosa matibabu.

Waziri huyo alisema kuwa bima hiyo ni chombo kinachovuja na ndiposa kitatupiliwa mbali na kutaja mpango mpya ambao utatekekezwa kupitia mamlaka ya SHA kama utakaosaidia Wakenya katika matibabu na kuboresha huduma za afya nchini.

Akizungumza katika eneo la Mwatate wakati wa uzinduzi wa mwezi wa uhamasisho wa saratani ya mlango wa Kizazi, Bi Nakhumicha alisema kuwa NHIF imekuwa ikikabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo ufisadi na udanganyifu haswa miongoni mwa wafanyakazi na vituo vya afya.

Alisema kuwa hali hii imesababisha Wakenya wengi wanaolipia bima hiyo kukosa huduma wanazostahili.

“NHIF ni kama chombo unachotekea maji na kina mashimo kwa hivyo hatuwezi kuendelea kukitumia. Tumekitupilia mbali na tukanunua kipya,” alisema.

Waziri huyo alisema kuwa kupungua kwa malipo ya mpango huo kutoka Sh500 hadi Sh300 kutawezesha Wakenya wengi kuweza kuingia ndani ya mpango huo.

“Itahakikisha kuwa kila Mkenya anapata huduma bora za afya bila kujali kipato chake. Mara hii lazima huu mpango utafanya kazi,” alisema Bi Nakhumicha.

Alisema kuwa mpango huo mpya utakuwa na vigezo vya kustahili ambavyo vitazingatia mahitaji ya Wakenya wote wakiwemo wasio na ajira, wazee, walemavu, na watoto.

“Nimekutana na wagonjwa wengi haswa wale wanaogua saratani. Wanasema kuwa wakitembelea vituo vya afya wanaambiwa mgao wao umeisha na kuambiwa waongeze pesa ili wapate matibabu,” alisema.

Bi Nakhumicha aliwataka Wakenya kujiunga na mpango huo akisema kuwa utakuwa na faida nyingi zikiwemo kupunguza gharama za matibabu, kuongeza upatikanaji wa huduma za afya, na kuimarisha afya ya umma.

Waziri alisema kuwa maafisa wa NHIF waliojihusisha na ufisadi kwa idara hiyo hawana nafasi ya kufanya kazi kwa mpango huo mpya. Alisema kuwa serikali itachukua hatua kali dhidi ya wote waliohusika na kuhujumu NHIF.

“Sina woga kusema kuwa wafisadi wote wa NHIF sitakubali waingie kwa huu mpango wa SHA. Nitatafuta wale wazuri wafanyie Wakenya kazi. Kama mtu analipia kadi yake akitaka matibabu lazima ayapate,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

Willy Pozee arejea kanisani baada ya miaka saba!

Mudavadi apeleka waraka wa habari njema Nyanza

T L