Ni kazi tu bila pesa lawama zikitanda baina ya Serikali, Cotu na waajiri
KWA mwaka mmoja, wafanyakazi wa Kenya wamekuwa wakifanya kazi wakiumia, sio tu kutokana na makato ya kodi yanayoendelea kuwaongezea mzigo wa kifedha, bali pia kwa kukosa nyongeza ya mshahara iliyotangazwa na serikali mwaka jana.
Licha ya Rais Ruto kutangaza nyongeza ya mshahara Mei 1 2024, imebainika kuwa baadhi ya waajiri hawajawahi kuitekeleza yakiwemo mashirika ya serikali.
Hata alipoongoza sherehe za mwaka huu jana katika uwanja wa Uhuru Gardens, Nairobi, kiongozi wa nchi hakutangaza nyongeza mpya ya mishahara kwa wafanyakazi wanaopokea malipo ya chini na badala yake akahimiza waajiri kutekeleza nyongeza ya asilimia sita aliyotangaza mwaka jana.
Dkt Ruto aliitaka Wizara ya Leba kuhakikisha kuwa nyongeza hiyo inatekelezwa kabla ya mipango mipya ya kuongeza mishahara kuanzishwa.
Hii inamaanisha wafanyakazi wa humu nchini wataendelea kuvumilia huku mapato yao yakiendelea kupungua na gharama ya maisha ikiendelea kupanda.
“Mwaka jana, tulikubaliana kuongeza mishahara kwa kiwango cha asilimia sita. Lakini inasikitisha kuwa, mjadala ulioibuka baadaye kiasi kwamba baadhi ya waajiri hawakutekeleza nyongeza hiyo, sasa nataka Wizara ya Leba kuhakikisha kuwa hilo linafanyika,” akasema.
Katibu Mkuu wa Muungano wa Wafanyakazi Nchini (COTU) Francis Atwoli alishutumu Shirikisho la Uajiri Nchini (FKE) kwa kutotekeleza nyongeza hiyo.
“Kwa kudharau agizo la Rais kwamba waongeze mishahara ya wafanyakazi, FKE, na wanachama wake wanahujumu sio tu wafanyakazi bali serikali ya Kenya,” Bw Atwoli akasema.
Akiongea wakati wa maadhimisho ya 59 ya Leba Dei mwaka jana, Rais Ruto alimwagiza aliyekuwa Waziri wa Leba, Florence Bore kuitisha mkutano wa wadau kujadili na kuelewana kuhusu nyongeza ya angalau asilimia sita ya mishahara kwa wafanyakazi wanaopokea mishahara ya chini zaidi.
Hata hivyo, ni hadi Oktoba mwaka jana ambapo Waziri Mutua aliunda Baraza la Kitaifa ya Mishahara kuanzisha mjadala kuhusu suala hilo.
Akijitetea jana, Afisa Mkuu Mtendaji wa FKE Jacqueline Mugo aliwaondolea lawama waajiri akisema, uamuzi kuhusu suala hilo unaweza tu kufanywa na baraza kama hilo linaloshirikisha wadau kutoka sekta mbalimbali za leba.
“Kwa hivyo, sio haki kwa wanachama wa FKE kulaumiwa kwamba, wamedinda kutekeleza nyongeza ya mishahara ya asilimia sita ilhali suala hilo lingali linashughulikiwa na Baraza la Kitaifa la Mishahara lililobuniwa na Waziri wa Leba Afred Mutua Oktoba 18, mwaka jana,” akaeleza kwenye mahojiana na wanahabari katika Uhuru Gardens.
Bi Mugo alisema kuwa shirikisho hilo liliwaagiza wanachama wake watekeleze uamuzi huo baada ya mabaraza ya mishahara kuundwa.
Aidha, alimshutumu Katibu Mkuu wa Cotu kwa kushirikiana na serikali katika kutekeleza sera ambazo, kwa maoni yake, zimewaumiza wafanyakazi na biashara.
“Ninajua ndugu yangu Francis (Atwoli) hatapendezwa na kauli yangu hii, lakini katika kila uamuzi wa sera tunaochukua — iwe ni kuongeza mshahara wa chini au kuanzisha ada mpya — tunapaswa kupata usawa wa kulinda ustawi wa wafanyakazi na pia kuruhusu biashara kukua,” alisema Bi Mugo.
Haya yanajiri huku wafanyakazi wa Kenya wakiendelea kukumbwa na hali ngumu ya maisha na ushuru mkubwa.
Jana, Bw Atwoli alitoa wito kwa serikali kubadilisha sheria inayohusiana na makato ya kisheria ya wafanyakazi.
Atwoli alisisitiza kuwa makato haya yanapaswa kuwa kwa mshahara wa msingi badala ya mishahara ya jumla, ili kutoa fursa kwa wafanyakazi kufurahia mapato ya kazi zao.
“Wafanyakazi wanajitahidi kufanya kazi, lakini baada ya makato, wanabaki na pesa kidogo au wanakosa chochote kabisa. Hii ni dhihaka kwa juhudi zao. Makato haya yanapaswa kufanywa kwa mshahara wa msingi ili mshahara wa jumla usiguswe,” alisema Atwoli, akionya kuwa hali hii inawafanya wafanyakazi wengi kuwa na hali ngumu ya kifedha, licha ya kufanya kazi kwa bidii.
Katika hotuba yake, Rais Ruto alipigia debe mipango tata ya serikali yake akisema imebadilisha maisha ya Wakenya. Alipuuza kauli za wakosoaji wa mpango wa nyumba nafuu akisema umesaidia kuunda nafasi 250,000 za ajira.