Ni kisasi tu Wanga akimvua naibu wake Oyugi Magwanga madaraka Homa Bay
UHASAMA kati ya Gavana Gladys Wanga na Naibu Gavana Oyugi Magwanga umefika kilele baada ya gavana kumtimua naibu huyo kama waziri wa kilimo wa Kaunti ya Homa Bay.
Kando na kuhudumu kama naibu gavana, Bw Magwanga ambaye ni mbunge wa zamani wa Kasipul amekuwa akisimamia wizara ya Kilimo.
Kwenye barua iliyonakiliwa kwa mawaziri wote wa kaunti, Mwanasheria Mkuu Fredrick Oregon na Katibu wa Kaunti Profesa Benard Muok, gavana alimwamrisha Waziri wa Barabara Danish Onyango kuhudumu pia kwenye wizara ya kilimo.
Mabadiliko hayo yamechochewa na hatua ya Bw Magwanga kumpinga gavana wazi na kumuunga mkono mwaniaji huru Philip Aroko katika kinyángányiro cha ubunge wa Kasipul.
Bi Wanga na wanasiasa wa ODM walikuwa wakimuunga mkono Boyd Were ambaye aliishia kushinda uchaguzi huo mdogo wiki jana.
Aidha, gavana hakumsaza Waziri wa Ardhi, Nyumba na Mipango Peter Ogolla ambaye anasemekana ni mwandani wa Bw Magwanga.
Kwenye wadhifa huo, Bi Wanga alimteua Joseph Mitito huku akisisitiza mabadiliko hayo yalifanyika kuhakikisha huduma bora kwa raia na kwa kufuata sheria.
“Kutokana na mamlaka niliyopewa namteua Danish Onyango kuhudumu wizara ya Barabara, Uchukuzi na Miundomsingi na pia awe kaimu waziri wa kilimo, unyunyuziaji mashamba maji na ufugaji. Mabadiliko haya yanaanza kutekelezwa mara moja,” ikasema notisi ya gavana.
Kando na uchaguzi mdogo wa Kasipul, Bi Wanga na Bw Magwanga walikuwa na uhasama mkubwa wa kisiasa 2022 kila moja akimezea mate ugavana.
Ilibidi aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga aingilie kati na kuwapatanisha ndipo Bw Magwanga akakubali kuwa mgombeaji mwenza wa Bi Wanga.
Naibu huyo wa gavana aligombea ugavana 2017 na akaangushwa na gavana wa wakati huo Cyprian Awiti. Alihudumu kama mbunge wa Kasipul kati ya 2007 hadi 2017.