Ni kweli, wakulima wameuziwa mbolea feki, Serikali yaungama ikiahidi kuishtaki kampuni
Na FATUMA BARIKI
Serikali sasa imekiri kwamba mbolea isiyo ya viwango sahihi vya ubora ilisambaziwa wakulima.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari Aprili 5, 2024, Wizara ya Kilimo inasema kwamba imefanya uchunguzi na ukaguzi wa mbolea zote na kwamba imebaini kwamba ni zile zilizotengenezwa na Ms KEL Chemicals zilizo na majina Kelphos Plus, Kelphos gold na NPK 10:26:10 pekee ndizo hazikuafikiwa viwango vya ubora.
Wizara inasema mbolea hiyo ilisambazwa kati ya Machi 5-10, 2024.
Kufuatia utambuzi huo, serikali imesema kwamba imechukua hatua kulinda sekta ya kilimo na wakulima kwa jumla kwa kusimamisha shughuli za kiwanda cha KEL Chemicals na kunyaka bidhaa zao zote zilizopatwa kuwa ghushi.
Aidha, imesema imenasa mbolea hiyo yote katika mabohari ya Bodi ya Mazao na Nafaka (NCPB) ili kusitisha usambazaji zaidi.
Serikali imetaka wakulima wote walio na mbolea za KEL Chemicals kusitisha mara moja matumizi yake na kuripoti katika afisi za NCPB walizo karibu nazo.
Wakati huo huo, wizara imesema shirika la kukadiria ubora wa bidhaa KEBS limeanzisha mchakato wa kisheria dhidi ya KEL Chemicals kwa kusambaza mbolea hiyo ya viwango duni.