Ni mazoea? Ghasia zarejea Kasipul wafuasi wa mirengo pinzani wakikomoana
MAUAJI ya aliyekuwa Mbunge wa Kasipul Charles Ong’ondo Were mnamo Aprili 30, 2025 yaliibua hofu kote nchini.
Eneo bunge hilo sasa limepoteza wabunge wawili wakiwa afisini. Wa kwanza alikuwa alikuwa Peter Owidi mnamo 2005 na kufuatiwa miongo miwili baadaye na Bw Were, matukio yanayoakisi ndoto za kisiasa katika eneo hili la Luo Nyanza.
Kwa miaka kadhaa, watu kadhaa wamepoteza maisha yao katika fujo za kisiasa eneo hilo huku wengine wengi wakipata majeraha mabaya.
Siku kadhaa kabla ya kuuawa kwa Bw Were, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Jamii ya Waluo Ker Odungi Randa, alielezea hofu kuhusu jinsi ghasia za kisiasa Kasipul ni tishio kwa maisha ya viongozi na wafuasi wao.
“Kifo cha Ong’ondo kiwe cha mwisho. Nawaomba viongozi wa jamii ya Waluo wanaosaka nyadhifa za kisiasa kutohusika katika umwagikaji wa damu. Sio jambo zuri kwa wanachama wa chama kimoja kupigana na kuuana, uovu huu ukome kabisa,” Bw Randa alisema baada ya kifo cha Bw Were.
Taifa Leo ilipomzungumzia Bw Randa Jumatano, wiki hii, siku moja baada ya fujo kutokea wakati wa kura ya mchujo ya ODM kati ya wafuasi wa Boyd Were na Newton Ogada, alionekana kuvunjika moyo.
Lakini aliendelea kuhimiza kwamba viongozi wa kisiasa washindane kwa amani bila kuchochea wafuasi wao kuzua fujo.
“Katika mashindano yoyote, sawa na ilivyo katika michezo, kuna washindi na wanaopoteza. Lakini kushindwa kwa kiongozi fulani hakupasi kuleta uhasama. Kubali kushindwa, mkumbatie mshindi na msonge mbele, fujo hazina maana,” akahimiza.
Kabla ya kuuawa kwake, marehemu Were alihusishwa na madai ya kuchochea fujo katika eneo bunge la Kasipul.
Ilidaiwa kuwa alizoea kutembea na kundi la vijana ambao waliwatisha na hata kuwashambulia wapinzani wake.
Hata hivyo, wandani wake walipuuzilia mbali madai hayo ambayo walidai yalichochewa kisiasa kwa lengo la kumharibia sifa.
Utulivu ulishuhudiwa katika eneo bunge hilo, kwa muda, baada ya kifo cha Were.
Lakini hali hiyo imevurugwa na fujo zilizokumba kura ya mchujo wiki hii, huku kukiibuka madai ya udanganyifu, vitisho na ghasia zilizosababisha uharibifu wa mali ya thamani kubwa.
Hii ni licha ya Baraza la Wazee wa Jamii ya Waluo kuhimiza amani na onyo kali kutoka kwa Waziri wa Usalama Kipchumba Murkomen.
Wanasiasa wengine pia walinaswa katika video wakitisha kufanya fujo, ishara kwamba umwagikaji wa damu huenda bado ukashuhudiwa Kasipul wakazi wanapojiandaa kuchagua mbunge mpya mnamo Novemba 27 mwaka huu.
Eneo bunge hilo lilibuniwa kutoka kwa eneo kubwa la Kasipul Kabondo mnamo 2012.
Katika uchaguzi mkuu wa 2013, Bw Oyugi Magwanga-Naibu Gavana wa sasa- ndiye alichaguliwa mbunge wa kwanza.
Lakini baada ya uchaguzi mkuu wa 2022, ushindani wa kisiasa ulishika kasi zaidi Kasipul na kuzaa fujo.
Hafla za mazishi na mikutano ya hadhara iligeuzwa uwanja wa vita kati ya wafuasi wa wanasiasa mahasimu.