Ni rasmi, Mswada wa Fedha 2024 umepitishwa Bungeni, sasa wasubiri kura ya mwisho
WABUNGE wamepitisha mswada tatanishi wa fedha kwa upesi ambao haujashuhudiwa awali, baada ya wabunge wa upande wa Upinzani kuondoa mapendekezo yao.
Mswada huo umepitishwa chini ya saa mbili, kufuatia wabunge wa upinzani kuondoa mapendekezo yao wakisema kwamba hawataki kushiriki kwa vyovyote katika uundaji wa sheria hiyo.
Hii inamaanisha kwamba mswada huo ambao umeibua pingamizi kote nchini kutokana na vipengele vya ushuru mpya, unapigiwa kura ya mwisho na ukipita kama inavyotarajiwa, utapelekwa Ikulu ya Nairobi kutiwa sahihi na Rais William Ruto na kuwa sheria wakati wowote wiki hii.
Haya yanajiri huku kukiwa na maandamano makubwa katika miji mbali mbali nchini na kampeni mitandaoni zilizotaka mswada huo ukataliwe wote ulivyo.
Kampeni hizo ziliendeshwa kwa heshitegi #RejectFinanceBill2024 na #OccupyParliament.
Alhamisi wiki jana, wabunge 204 wanaoegemea mrengo wa serikali walipiga kura kuuvukisha hadi kwa hatua ya tatu na ya mwisho, ambayo ilikuwa ya leo Jumanne ambapo vipengele kadhaa vilikuwa vinapigiwa kura ikiwemo vile vilivyohusu ushuru wa mkate na magari.
Habari zaidi ni kadiri tunavyozipokea…