Habari za Kitaifa

Ni ushindi mkubwa kwa walimu wakipata donge nono

Na  NDUBI MOTURI July 19th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Walimu kote nchini wanatarajiwa kupokea nyongeza ya mishahara kati ya asilimia 5 hadi 29.6 kufikia mwisho wa mwezi huu, kufuatia kutiwa saini kwa makubaliano mapya kati ya Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) na vyama vitatu vikuu vya walimu — Chama cha Walimu wa Shule za Sekondari (KUPPET), Chama cha Kitaifa cha Walimu (KNUT), na Chama cha Walimu wa Mahitaji Maalum (KUSNET).

Makubaliano hayo, yatakayotumika kwa muda wa miaka minne, yatagharimu serikali jumla ya Sh33.8 bilioni, ambazo zitagawanywa kwa usawa kila mwaka, huku walimu wakipokea nyongeza kila mwaka.

Kwa mujibu wa viongozi wa vyama vya walimu, hatua hiyo ni ushindi mkubwa unaorejesha heshima ya taaluma ya ualimu na kuondoa tofauti za muda mrefu katika viwango vya malipo.

Makubaliano hayo yalitiwa saini Ijumaa katika Taasisi ya Elimu ya Mahitaji Maalum (KISE) mtaa wa Kasarani, Nairobi, baada ya mazungumzo yaliyochukua muda mrefu hadi usiku.

Mabadiliko hayo si tu ya kifedha, bali pia yanahusisha sera mpya kama vile mchakato wa haraka wa pensheni, na ulinzi kwa walimu wa kike wanaonyonyesha.Marekebisho ya mishahara yataanza kutekelezwa Julai 1, 2025, huku mishahara ya mwezi huo ikitarajiwa kuakisi viwango vipya mwishoni mwa mwezi.

Kwa upande wa KNUT, chama kinachowakilisha hasa walimu wa shule za msingi, nyongeza ya mishahara itakuwa kati ya asilimia 12 hadi 29.5, huku walimu wa ngazi za chini wakipata ongezeko kubwa zaidi.

Katibu Mkuu wa KNUT, Bw Collins Oyuu, alisema kuwa makubaliano hayo ni kati ya nyongeza muhimu zaidi kuwahi kupatikana katika miaka ya hivi karibuni.

“Walimu wa ngazi za chini sasa wana kila sababu ya kutabasamu. Wamepewa kipaumbele. Na suala tata zaidi — mwongozo wa maendeleo ya kazi — sasa utapitiwa upya,” alisema Bw Oyuu.

Aidha, alisema kuwa maeneo yenye mazingira magumu yaliyotangazwa awali hayataathiriwa, na pensheni kwa walimu wanaostaafu itashughulikiwa kwa haraka zaidi.

Alisisitiza haja ya kuwepo kwa sheria mpya kupitia Mswada wa Marekebisho ya Tume ya Huduma kwa Walimu, ili kuimarisha mazungumzo ya baadaye.